Friday, August 30, 2013

TRAFIKI FEKI ALIYEKAMATWA SIKU CHACHE ZILIZOPITA KUMBE NI MFUNGWA WA GEREZA LA ISANGA DODOMA



MAZITO tena yameibuka kuhusu yule trafiki feki James Hussein, mkazi wa Kimara Matangini, jijini Dar es Salaam ambaye yuko Gereza la Segerea, Dar akikabiliwa na kesi ya kujifanya askari wa usalama barabarani.

Habari za ndani kutoka Gereza la Isanga, Dodoma zinadai kuwa, trafiki huyo ana mambo mengi ya kushangaza ambayo Watanzania wengi hawayajui.

Mtoa habari wetu alisema kuwa, James Hussein si jina halisi la trafiki feki huyo. Alisema jina lake halisi ni Ali Kinanda.

“Yule jamaa anaitwa Ali Kinanda, sisi kumwona kwenye picha gazetini akijiita James Hussein tulishangaa sana,” kilisema chanzo chetu.

Chanzo kikazidi kudai kwamba, kuanzia mwaka 1984 jamaa huyo alikuwa ni askari magereza katika Gereza la Butimba, Mwanza hadi mwaka 1987 alipoacha.

Mtoa habari wetu aliendelea kumwanika trafiki feki huyo kuwa, mwaka 2002 mtuhumiwa huyo alidaiwa kupata msala wa tukio la ujambazi lililotokea Mpwapwa, Dodoma ambapo kesi yake iliunguruma hadi mwaka 2003 ambapo hukumu ilitolewa yeye na wenzake kwenda jela miaka 30.

“Mwaka 2002 mpaka 2003, Kinanda alipata kesi ya ujambazi akiwa na wenzake, sikumbuki idadi yao. Kesi iliisha kwa hukumu ya miaka 30 jela kwenye Gereza la Isanga hapa Dodoma,” alisema mnyetishaji huyo.

“Akiwa gerezani, Kinanda alionekana mtiifu kiasi kwamba alipewa cheo cha kusimamia wenzake, yaani mnyapara wakiamini anaendelea vizuri na kifungo chake hicho.

“Hakuna aliyejua kama jamaa anaweza kutoroka. Ama kweli moyo wa mtu anaujua mwenyewe. Hivi hapa (Gereza la Isanga) wafungwa wenzake wameshangaa kusikia jamaa amekuwa trafiki huko Dar es Salaam,” kilidai chanzo.

Habari zaidi ziliendelea kudai kwamba, Desemba 10, 2012 akiwa gerezani, mfungwa huyo alitoroka katika mazingira ya kutatanisha akiwa chini ya uangalizi wa askari magereza aliyejulikana kwa jina moja la Shaibu.

Ilidaiwa kuwa, baada ya picha yake kuonekana kwenye gazeti, askari magereza wa Isanga waliutaarifu uongozi mara moja ambapo nao ulituma wachunguzi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza mchakato wa kumtia mikononi mfungwa huyo ili akamalizie kifungo chake cha miaka thelathini jela.

Inadaiwa kuwa, wachunguzi hao ambao ni askari magereza wapo Dar wakisubiri siku ya kesi ya kujifanya trafiki itakapopelekwa kusikilizwa kwa hakimu.

Wakati mnyetishaji wetu kutoka gerezani Isanga Dodoma akianika madai ya siri hiyo nzito, Agosti 26, mwaka huu jijini Dar es Salaam, Mwandishi Wetu, alipata taarifa kuwa, mtuhumiwa huyo wa kutenda kosa la kujifanya trafiki amefariki dunia ghafla akiwa gerezani Segerea.

Ilibidi mwandishi wetu amtafute Msemaji wa Jeshi la Magereza Tanzania, Meja Mtiga Omar na kumuuliza kuhusu madai hayo ya kifo ambapo alisema:

“Si kweli kwamba amekufa, bali ana tuhuma nyingine ya kutoroka gerezani ambapo tutamfungulia mashitaka mengine ya kutoroka akiwa gerezani anatumikia kifungo chake.”

Juhudi za kumpata Mkuu wa Gereza la Isanga, Dodoma zilishindikana baada ya simu yake ya mkononi kuita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

James Hussein kama ndiye Ali Kinanda yupo Gereza la Segerea, hadi Septemba 5, 2013 kesi yake itakaporudi tena mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Joyce Minde kwa ajili ya kusikilizwa.