MIHADHARA ya dini iliyokuwa imepigwa marufuku na Serikali imeruhusiwa
kuendelea kwa masharti ya kutojihusisha na mahubiri yanayolenga
kupandikiza chuki miongoni mwa Wakristo na Waislamu. Serikali pia
imewataka viongozi wote wa dini kuwakataa na kuwapiga marufuku watu
wanaojiingiza katika nyumba za ibada huku wakiwa na malengo ya siasa.
Akizungumza katika kongamano la Umoja wa Wahadhiri wa dini za
Kikristo na Kiislamu Dar es Salaam juzi, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo
wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja alisema Serikali haiwezi kuingilia
shughuli za dini kama zinaendeshwa kwa ustaarabu bila kuvunja sheria.
Chagonja
ambaye alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Dk. Emanuel
Nchimbi alisema Serikali haijawahi kupiga marufuku mihadhara yoyote
inayoendeshwa bila kusababisha vitendo vya chuki na uhasama kwa
Watanzania.
Kuruhusiwa kwa mihadhara hiyo kumekuja ikiwa imepita
zaidi ya miezi minane tangu Serikali ilipopiga marufuku mihadhara hiyo
nchi nzima ikiwa ni hatua ya kukabiliana na machafuko ya dini yaliyokuwa
yanalinyemelea taifa.
Uamuzi huo ulichukuliwa siku chache baada
ya baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu kujiandaa kuandamana kwenda
Ikulu kutaka atolewa rumande Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu,
Sheikh Ponda Issa Ponda.
Katika kongamano la juzi, Chagonja
aliwaasa viongozi hao kuwa na mfumo mpya wa dhana ya uhalisia ya
kutangaza dini na kuacha kukejeliana kati ya dini moja na nyingine
kuepuka vitendo vya chuki za dini.
Kiongozi wa Mihadhara ya
Kiislam, Naibu Amir, Shekh Rajabu Salum, alisema mihadhara ya pande zote
mbili ijulikanayo kama ‘mihadhara linganishi’ haijawahi kuwa tishio la
amani nchini.
Naye Mwenyekiti wa mihadhara ya Kikristo,
Mwinjilisti Daniel Mwankemwa alisema mihadhara yao imetoa mchango mkubwa
kwa waumini wao kuimarika kiroho baada ya kupata ufafanuzi sahihi wa
hoja mbalimbali zilizokuwa zikiwasumbua.