RAISI WA MALAWI AAMUA KUMISIFIA LIVE RAIS WA TANZANIA KWA KUIMARISHA AMANI,DEMOKRASIA NA USALAMA KATIKA JUMUIYA..!
Rais Kikwete akiteta jambo na dk
Joyce Banda pamoja na rais wa msumbiji Armando Guebuza wakati wakitoka
nje na viongozi wengine kwenye mkutano wa SADC
RAIS wa Malawi, Joyce Banda amempongeza
Rais Jakaya Kikwete kwa kuimarisha demokrasia, amani na usalama katika
nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za kusini mwa Afrika (SADC).
Banda alitoa pongezi hizo jana wakati
akihutubia Mkutano wa 33 wa Wakuu wa SADC baada ya kukabidhiwa nafasi ya
uenyekiti wa jumuiya hiyo kutoka kwa Rais wa Msumbiji, Dk Armando
Guebuza.
“Wananchi wa Malawi, mimi na SADC
tunampongeza Kikwete kwa kuimarisha amani, demokrasia na usalama katika
jumuiya katika kipindi chake cha uongozi (wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na
Usalama),” alisema.
“Pia Rais wa Msumbiji, Armando Guebuza
katika uongozi wake wa uenyekiti alishirikiana na Kikwete kushughulikia
matatizo ya kisiasa na kuufanya ukanda wa nchi za SADC kuwa na amani,”
alisema Rais Banda, ambaye nchi yake ina mgogoro na Tanzania juu ya
mpaka wa Ziwa Nyasa.
Mgogoro huo uliibuka baada ya Serikali
ya Malawi bila kushauriana na Tanzania, kutoa leseni kwa kampuni mbili
za kigeni, kutafuta mafuta katika eneo la Ziwa upande wa Tanzania.
Chanzo cha mgogoro huo unaoshughulikiwa
na jopo la marais wastaafu wa Afrika; Thabo Mbeki (Afrika Kusini),
Joachim Chisano (Msumbiji), Festus Mogae (Botswana) na wanasheria saba
wa kimataifa, ni mikataba yenye utata iliyoachwa na wakoloni.
Sifa za Kikwete
Katika kipindi cha mwaka mmoja cha
uongozi wa Rais Kikwete katika asasi hiyo ya siasa, ulinzi na usalama
aliweza kufanikisha kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Zimbabwe, ambao
Robert Mugabe ameshinda.
Amefanikisha pia kuanza kwa mchakato wa amani na kupatikana kwa muafaka wa kisiasa nchini Madagascar.
Pia katika kipindi chake, alifanikisha
kupelekwa kwa wanajeshi wa kulinda amani katika mji wa Goma, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambapo waasi wa M23 wanapambana na wanajeshi
wa serikali. Wanajeshi hao wa kulinda amani wametoka Tanzania, Malawi
na Afrika Kusini.
Rais Kikwete amekabidhi madaraka hayo
jana kwa Rais wa Namibia, Hifikepunye Pohamba. Banda aahidi amani
Akizungumzia mkakati wake wakati wa uongozi wake wa mwaka mmoja kama
Mwenyekiti wa SADC, Banda alisema ili ukanda wa SADC uwe na amani na
usalama ni lazima nchi wanachama zipambane na umasikini.
“Lazima tuimarishe siasa za ndani za
nchi zetu, tuwe wavumilivu wa kisiasa na tusaidie wanawake wasiwe
nyuma,” alisema. Aliahidi kuimarisha jumuiya za kikanda pamoja na kilimo
kwa maelezo kuwa kilimo ndicho mwajiri mkuu wa wananchi wa nchi za
SADC.
“Nitahamasisha kilimo kiboreshwe ili
wananchi wa SADC waweze kuendesha kilimo cha biashara na pia sekta
binafsi waingie kwenye kilimo na tupate masoko mapya ya bidhaa za kilimo
nje ya mipaka ya ukanda wetu”.
Alitaka katika ukanda wa jumuiya ya SADC
kuboreshwe mwingiliano wa wananchi wa nchi za ukanda huo. Alisema
haiwezekani kuboreshwa kwa jumuiya za kikanda bila kuruhusu mwingiliano
huru wa wananchi wake.
Rais Banda alitaka wanawake wapewe
nafasi katika uongozi na kujengewa uwezo katika kuimarisha uchumi na
kuondokana na umasikini na kusisitiza kuwa, “wanawake ndiyo wanaopambana
na umasikini, wanabakwa, wanakabiliwa na unyanyasaji na wengi
wamepoteza utu wao”.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya
Umoja wa Afrika (AU), Dk Nkosazana Dlamini- Zuma alizitaka nchi za
Afrika kuimarisha miundombinu ili mazao ya wakulima yaweze kusafirishwa
pamoja na kuboreshwa kilimo, uwekezaji na kujengwa kwa viwanda.
“Lazima tufanye kazi pamoja
kuwahakikishia chakula watu wetu wa SADC na Afrika haiwezi kuendelea
bila kuweka wanawake kila maeneo na kutafuta ufumbuzi wa changamoto
zinazotukabili za tatizo la ajira kwa vijana, umasikini, sekta duni ya
viwanda na tatizo la kutokuwepo usawa wa kijinsia,” alisema Zuma.