AUAWA KIKATILI APIGWA NA KISHA ACHOMWA MOTO BAADA YA MPENZI WAKE KUMWITA MWIZI.
Mzozo wa wapenzi wawili usiku,
umesababisha mmoja wa kike kupiga mayowe ya kumuita mwenzake mwizi,
akavamiwa na watu waliompiga na kumchoma moto hadi kufa.
Kisa hicho kimetokea mkazi wa Magazini
mjini Mpanda mkoani Katavi, Florence Mabuga (29), ambaye baada ya
kuvamiwa na watu akidhaniwa mwizi, alipigwa na kuuawa na mwili wake
kuchomwa moto mbele ya nyumba yake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi,
Dhahiri Kidavashari, amethibitisha kuuawa kwa mkazi huyo katika kisa
hicho kilichotokea katika mtaa wa Nsemulwa-Magazini hivi karibini, usiku
wakati Mabuga akimsindikiza mpenzi wake wa kike akitokea nyumbani
kwake.
Akisimulia mkasa huo wa kusikitisha,
Kamanda Kidavashari alisema Mabuga ambaye alikuwa msimamizi wa vibarua
wa kujenga nyumba mjini humo, siku hiyo baada ya kurejea nyumbani,
alitembelewa na mpenzi huyo ambaye jina lake halijafahamika.
Inadaiwa wakati Mabuga akimsindikiza
rafiki huyo, ulizuka mzozo baina yao ambapo Mabuga alitishia kuwa usiku
huo angechoma nyumba ya rafiki huyo, ndipo kwa hasira na hofu ya
kuchomewa nyumba, alipiga yowe akiashiria kuwa Mabuga ni mwizi.
Kwa mujibu wa Kidavashari, Mabuga
alianza kutimua mbio mara alipoona kundi la wananachi wenye hasira
wakiwa na silaha mbalimbali za jadi wakikimbilia alipokuwa amesimama na
rafiki yake huyo.
Inadaiwa kuwa wananchi hao walifanikiwa
kumkamata Mabuga aliyekuwa akijaribu kuingia ndani ya nyumba yake, na
kuanza kumpiga na kumsababishia mauti.
“Uchunguzi wa awali wa kipolisi
umebaini kuwa Mabuga alisingiziwa tu na mpenzi wake huyo, kwani hakuiba
kitu chochote, ila mpenzi wake huyo alimpigia mayowe ya mwizi baada ya
kuzuka mzozo baina yao,“ alidai.
Kwa mujibu wa Kidavashari mtuhumiwa
huyo anaendelea kusakwa ili sheria ichukua mkondo wake, pia hakuna mtu
yeyote aliyekamatwa hadi sasa kwani wananchi hao walikimbia eneo la
tukio mara baada ya kufanya unyama huo.
via habari leo