Kaka mtu akitiwa mbaroni
MWANAFUNZI wa kidato cha pili jina kapuni (16), amejikuta akiozeshwa na wazazi wake kwa mwanaume aliyetambulika kwa jina la Kaizilege Jabiri (31) ambaye ni mtoto wa mama yake mkubwa...
Tukio hilo lilitokea Juni 14, mwaka huu jijini Dar nyumbani kwao Mlandizi, Bagamoyo, Pwani ambako mwanaume huyo alifunga ndoa na binti huyo na kurejea naye nyumbani kwake, Ubungo Kisiwani, Dar huku baadhi ya watu wakihofia uhai wa ndoa hiyo.
Baada ya kuanza maisha ya ndoa kama mke na mume, Agosti 6, mwaka huu taarifa zikafika kwenye Kituo cha Polisi cha Ubungo ambapo maafande walisema hiyo haiwezekani.
“Polisi walipopata habari walisema hakuna ndoa hapo, wakajipanga kwenda kuvamia nyumbani kwa wanandoa hao,” kilisema chanzo.
Dada mtu akiwa ameshika tama.
Chanzo kiliongeza kuwa, nje ya nyumba hiyo walimkuta msichana huyo anapika huku kaka yake akiwa kajipumzisha ndani akisubiri lishe hiyo.
Kaizilege alipobanwa alikiri kuwa mwanafunzi huyo ni mkewe walifunga ndoa ya Kiislamu, Mlandizi. Kwa kuwa kisheria ni kosa kuoa mwanafunzi aliye chini ya miaka 18 alilazimika kupelekwa Kituo cha Polisi, Magomeni, Dar.
Kwa upande wake mwanafunzi huyo alikiri kuolewa na kaka yake. Alisema yeye ni mwanafunzi, yuko kidato cha pili Mlandizi. Alisema hakuwa na maamuzi ya kuikataa ndoa hiyo kwani uwezo huo ni wa wazazi wake.
Denti huyo alizidi kuweka wazi kwamba, chanzo kikubwa cha kuozeshwa kwake ni kutokana na ugumu wa maisha ulioko katika familia hali iliyomsukuma baba yake mzazi kumshawishi aolewe na kaka yake.
Alisema kuwa aliambiwa atakapoolewa, mumewe huyo angeendelea kumsomesha jambo ambalo halikufanyika.
‘’Mimi nilikubali niolewe ili baadaye nipelekwe shule kwani wazazi wangu hawana pesa za kunisomesha na mimi siwezi kukataa kwa sababu wazazi ndiyo wameamua,’’ alisema.
Hata hivyo, kwa mujibu wa baadhi ya ndugu, dini ya wawili hao inaruhusu kumuoa mtoto wa mama’ke mkubwa endapo atakuwa amefikisha umri wa miaka 18 haki ambayo kwa mwanafunzi huyo haipo.
Mwandishi wetu aliwasiliana na msemaji wa dawati la jinsia Wilaya ya Kinondoni, Dar, Inspekta Prisca Komba ambapo mhusika mmoja alisema:
‘’Kwa mujibu wa sheria na taratibu za utamaduni wetu si ruhusa kuoa mtoto wa mama mkubwa tena akiwa bado mwanafunzi, mimi naona ni kuvunja sheria na ni lazima huyu bwana afunguliwe jalada la uchunguzi.”
Kaizilege amefunguliwa jalada la uchunguzi kwa Kumbukumbu MAG/RB/9015/2013, mara uchunguzi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.