RAIS Paul Kagame wa Rwanda, sasa hayupo tayari kukanyaga ardhi ya
Tanzania kutokana na kile kinachoonekana kuwa ni mgogoro wa kidiplomasia
unaoendelea kati yake na Rais Jakaya Kikwete.
Wakati hayo yakifikia hapo, kikao cha Bunge la
Afrika Mashariki (EALA), linakoketi mjini Arusha kilivunjika baada ya
Spika wa bunge hilo, Magreth Zziwa, kugongana kauli na Mbunge mmoja wa
Rwanda jambo lililosababisha wabunge wote wa Rwanda kususia kikao na
kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.
Mwenendo wa hayo yaliyojitokeza
jana katika Bunge la Afrika Mashariki hadi kikao kuvunjika, msingi wake
ni mgogoro unaowagusa wakuu hao wawili wa dola.
Habari
zilizolifikia gazeti hili toka katika vyanzo vyake mbalimbali vilivyo
ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, lakini pia katika vikao vya Bunge
hilo la Afrika Mashariki vinavyoendelea jijini Arusha zinaeleza kuwa,
Rais Kagame hata kama ataalikwa kuja nchini leo, hatakuja.
MTANZANIA Jumatano limedokezwa kuwa jambo hilo tayari limethibitishwa na Wabunge wa Rwanda wanaohudhuria vikao vya (EALA).
Taarifa
toka ndani ya Bunge hilo zilizolifikia MTANZANIA Jumatano zinaeleza
kuwa, tayari mzimu wa msigano huo uliojitokeza baina ya wakuu hao wawili
wa dola, umeanza kuwavuruga wabunge hao baada ya jana kikao cha Bunge
hilo kuvunjika, kutokana na kuibuliwa kwa hoja ya kutaka vikao vya Bunge
hilo kufanyika kwa utaratibu wa kuzunguka kila nchi.
Zinaeleza
zaidi kuwa; Ni katika hoja hiyo wabunge wa Kenya na Rwanda walionekana
kuungana na kuwa kitu kimoja na hivyo kususia kikao hicho cha jana,
jambo ambalo lilimlazimisha Spika wa Bunge hilo, Magreth Zziwa kuvunja
kikao.
HALI ILIVYOKUWA
MTANZANIA Jumatano limedokezwa kuwa,
wabunge hao walianza kutoka ndani ya kikao kilichokuwa kikiendelea jana,
baada ya mmoja wa wabunge hao kutoka Rwanda, James Ndahiro kuomba
mwongozo kwa Spika.
Habari zinaeleza kuwa chanzo cha mbunge huyo
wa Rwanda kuomba mwongozo, kilitokana na Mbunge kutoka Kenya, Peter
Mathuki kutoa hoja ya kutaka suala la vikao hivyo kufanyika kila nchi
wanachama, lijadiliwe.
“Sasa baada ya mbunge huyo wa Kenya kutaka
suala la vikao vya Bunge kufanyika kila nchi wanachama yaani ‘rotation’
lijadiliwe pale kikaoni, Spika akamwambia hilo ni jambo la haraka sana
na ikizingatiwa imebaki wiki moja vikao viishe na kwamba kama anataka
lizungumziwe, alilete kama ‘motion’.
“Baada ya Spika kujibu
hivyo, ndipo mbunge wa Rwanda akaomba mwongozo kwa Spika…Spika akamjibu
kwamba anataka mwongozo gani tena wakati ameshamjibu yule wa Kenya,
ndipo wabunge wa Rwanda wakatoka ndani ya kikao wakisema hawataki
kuburuzwa huku wakifuatiwa na wa Kenya.”
Taarifa zaidi zilieleza
kuwa kitendo hicho ambacho kilisababisha kikao kuvunjika, kilikwamisha
kuapishwa kwa Waziri mpya wa EALA kutoka Rwanda.
Ilielezwa kuwa baada ya wabunge hao kutoka, Spika aliahirisha kikao kwa kutumia kanuni kwamba, baada ya dakika 15 warudi.
“Baada
ya dakika 15 tuliporudi, wabunge wakawa wachache huku wale wa Rwanda na
Kenya hawakurudi tena na waliorudi walikuwa jumla 13 pamoja na Spika
kati ya wabunge 45. Ndipo Spika akasema hatuwezi kuendelea na kikao
kutokana na uchache wa wabunge, hivyo kikaahirishwa hadi kesho (leo),”
kilisema chanzo chetu hicho.
Hata hivyo wakati hayo yanajitokeza,
utaratibu wa vikao vya Bunge la Afrika Mashariki unaelekeza kuwa
vitafanyikia Arusha ambako ni makao makuu.
Habari zilizolifikia
gazeti hili zinaeleza kuwa, Kamati ya kuratibu Mambo ya Bunge
iliyokutana Entebe Uganda, ilipanga kuwa kwa mwaka vikao vya Bunge
vitakuwa sita huku vitatu vikifanyika Arusha ambako ni makao makuu,
kimoja Nairobi na vingine viwili bado haijajulikana.
Pamoja na
Kamati kufikia uamuzi huo, bado inaelezwa kuwa baadhi ya wabunge
wanapinga vikao hivyo kuendelea kufanyika na hasa wa Rwanda ambao
inadaiwa kuwa wamepewa maagizo fulani kutoka kwenye Serikali yao
Mbali
na hilo la vikao, nyufa nyingine zinazoelezwa kuhatarisha msingi wa
Bunge hilo, ni kile kinachodaiwa kuwapo kwa utendaji wa upendeleo wa
Spika, Margaret Zziwa.
Kwamba Spika Zziwa amekuwa akishutumiwa kupanga safari za nje kwa upendeleo na kwamba hazieleweki zinapangwaje.
KAGAME KUTOKANYAGA TANZANIA
Wakati hayo yakijiri, imeelezwa
kuwa hata Rais Kagame, akialikwa kuhutubia vikao vya Bunge hilo,
hataweza kuja nchini kutokana na mgogoro uliopo.
Taarifa
zilizolifikia gazeti hili toka ndani ya bunge la EALA, zinaeleza kuwa
wabunge kutoka Rwanda wananung’unika vikao kufanyika Arusha na wameeleza
bayana kwamba itakuwa vigumu kwa rais wao kuja hapa nchini endapo
ataalikwa na Spika wa Bunge hilo kuja kuhutubia katika vikao hivyo.
“Kwa
kawaida vikao vya bunge vinapofanyika, mara nyingi anayehutubia vikao
ni Mwenyekiti wa EAC, ambaye kwa sasa ni Yoweri Museveni na rais wa nchi
ambako vikao vinafanyika, lakini wakati mwingine spika anaweza akaamua
na kumteua rais kutoka nchi yoyote.
“Sasa Spika akimteua Kagame
ni dhahiri itakuwa ngumu kuja Tanzania kutokana na mgogoro unaoendelea
baina yake na Rais Kikwete,” kilisema chanzo chetu hicho cha habari.
Msigano
wa kauli baina ya viongozi hao wakuu wa dola, ulijitokeza baada ya Rais
Kikwete kutoa ushauri kwa Rais Kagame wa kukaa meza moja na waasi wa
FDLR.
Hata hivyo baada ya siku chache, Kagame alinukuliwa na
vyombo mbalimbali vya habari nchini Rwanda akimkejeli Kikwete hadi
kufikia kutoa kauli zenye vitisho dhidi yake.
Tangu Rais Kikwete alipotoa ushauri huo, Kagame amekuwa akiendelea kutoa lugha zisizo na staha kwa Tanzania.
Baadhi
ya vyombo vya habari nchini Rwanda, navyo vimekuwa na mwelekeo huo huo,
ambapo hivi karibuni vilianza kuhusisha ushauri huo wa Rais Kikwete
kuwa msingi wake unatokana na undugu uliopo kati ya mke wake, Mama Salma
Kikwete na wabaya wa Kagame.
Kwamba mke wa Rais Kikwete ni
binamu wa kiongozi wa zamani wa Rwanda, Juvenal Habyarimana, habari
ambazo zimekanushwa vikali na Serikali.
Ni katika mwenendo huo
huo, wiki iliyopita ilibainika kuwa Rwanda na Uganda zinakusudia
kutangaza kujitoa kutumia Bandari ya Dar es Salaam kuanzia mwezi ujao.
Katika
hilo, leo Marais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Museveni wa Uganda
pamoja na Paul Kagame wa Rwanda, wanatarajiwa kuzindua Gati ya bandari
ya Mombasa yenye thamani ya dola za Marekani milioni 66.7 ambayo ni
zaidi ya Sh bilioni 100 za Kitanzania.
Bandari hiyo ambayo
itaongeza uwezo kwa asilimia 33, Rais Museveni ambaye ni Mwenyekiti wa
Jumuiya Afrika Mashariki (EAC), ataongoza zoezi hilo la uzinduzi.
Baadhi
ya wachambuzi wa sayansi ya kiuchumi, wanasema kuwa endapo Rwanda na
Uganda zitajitoa kutumia bandari ya Dar es Salaam, hizo zitakuwa ni
habari mbaya kwa nchi.