Friday, July 5, 2013

WAZIRI MKUU MSTAAFU LOWASA AVIFUNGUKIA VYOMBO VYA DOLA

WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowassa amevitaka vyombo vya dola na wafanyabiashara wakubwa nchini, kujenga mahusiano bora kati yao na wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga) ili kuondoa tabaka la matajiri na masikini linaloweza kuathiri uchumi wa taifa.

Lowassa aliyasema hayo jana wakati akizungumza na machinga wa eneo la Makoroboi jijini Mwanza, ambao pamoja na mambo mengine aliwachangia sh milioni 20 kwa ajili ya kutunisha mfuko wao.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni mbunge wa Monduli, aliinyoshea kidole Serikali ya chama chake cha Mapinduzi (CCM) na kuitaka ihakikishe inatekeleza kwa vitendo ilani yake inayosisitiza wananchi kuwezeshwa kiuchumi ili kuondoa matabaka.

Huku akishangiliwa na wafanyabiashara hao, Lowassa ambaye aliongozana na baadhi ya makada wa CCM kutoka ndani na nje ya Mwanza, alisema kila mwananchi wa Tanzania lazima ale, ingawa kwa namna tofauti.

Alisema kuwa ili amani iwepo nchini, lazima Jeshi la Polisi na wafanyabiashara wakubwa wawathamini wafanyabiashara wadogo.

“Tunataka tuwasaidie hawa vijana wetu, maana ni nguzo kubwa sana katika maendeleo ya taifa. Ilani ya CCM inasema lazima watu wawezeshwe kiuchumi.

“Kwa maana hiyo katika nchi yetu kila mtu lazima ale. Na kula kwenyewe tunatofautiana, huyu anakula mkate na huyu anakula hiki. Na ili amani iwepo lazima RPC au OCD na wafanyabiashara wawathamini machinga,” alisema Lowassa.

Pia alitahadharisha kuwa endapo wafanyabiashara hao wadogo watadharauliwa katika nchi, lazima watakula sahani moja na matajiri.

Alitumia pia fursa hiyo kukanusha tuhuma dhidi yake kwamba amejilimbikizia mali.

“Wapo baadhi ya watu wanasema hela ninazotoa hizi ni zangu. Mimi sina fedha, ninazotoa ninapewa na marafiki zangu. Mimi si tajiri wa fedha, ila ni tajiri wa marafiki na ushawishi ninao,” alitamba.

Katika hatua nyingine, Lowassa alikataa kuulizwa maswali na wamachinga hao akisema ameandaa kamati itakayoratibu harambee ya kuwachangia kwa lengo la kupata sh bilioni moja.

“Kwa maandalizi ya harambee nitakayorudi tena kuifanya, na ili mjue kwamba nipo makini natoa hundi ya sh milioni 10 na milioni 10 nyingine nitaitoa leo hii,” alisema Lowassa ambaye baadaye aliondoka kwa kutembea kwa miguu hadi Mwanza Hotel.