Friday, September 6, 2013

VURUGU ZINAZOENDELEA BUNGENI WANANCHI WANASEMA NI MASLAI YA VYAMA BINAFSI


Baada ya kuibuka mvutano mkali bungeni jana, kati ya Naibu Spika, Job Ndugai na wabunge wa Kambi ya Upinzani, wasomi, wanaharakati, Chama cha Madaktari Tanzania (Mat), Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), vimesema kinachoendelea sasa ndani ya Bunge ni masilahi ya vyama vya siasa siyo taifa.


Walitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuwataka askari kumtoa nje ya Ukumbi wa Bunge, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.


Mbowe aligoma kukaa chini na kuungwa mkono na wabunge wa upinzani, akishinikiza kuahirishwa kujadiliwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, hadi hapo Zanzibar itakaposhirikishwa, muda mfupi baada ya wabunge kupiga kura na 156 kutaka ujadiliwe na 56 wakitaka uondolewe.


Wabunge hao wa upinzani kutoka vyama vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi, juzi walitoka nje ya Ukumbi wa Bunge wakishinikiza kuahirishwa kujadiliwa kwa muswada huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally alisema mvutano huo umejaa masilahi ya wanasiasa kwa kila upande kujaribu kuvutia kwake.


“Mvutano ule hauzungumzi kabisa mwafaka wa Bunge la Katiba, binafsi nadhani Bunge la Katiba linatakiwa kuwa na wabunge wapya kabisa na wasiotoka katika chama chochote cha siasa,” alisema


Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya alisema: “Marekebisho hayo yanafanyika kwa ajili ya mustakabali wa Muungano wetu, kama Zanzibar hawakushirikishwa, uwekwe utaratibu wa jambo hilo kufanyika ili kipatikane kitu bora, siyo bora Katiba.”


Alisema nchi zilizoendelea zimepata mafanikio kwa kuwa zina Katiba nzuri ambazo zinaweza kudumu kwa miaka 100 kabla ya kufanyiwa marekebisho..