Serikali
ya Rwanda imetoa tamko linaloonyesha kutoielewa kauli ya Rais Jakaya
Kikwete, iliyoamuru wahamiaji haramu kuondoka nchini, hali inayoonekana
kukwepesha hoja.
Rwanda
kupitia waziri wake wa Mambo ya Nje, Louise Mushikiwabo, ilikaririwa
ikieleza kwamba hawatajibu mapigo agizo la Rais Jakaya Kikwete ya
kuwataka Wanyarwanda wote waliolowea Magharibi mwa Tanzania kuondoka
haraka.
Mushikiwabo
alisema wako tayari kuwapokea na kuwalinda wote waliofukuzwa Tanzania
kwa kisingizio kuwa ni wahamiaji haramu, akieleza kwamba anasikitishwa
kwa kuwa Tanzania haikufanya jitihada yoyote kuwasiliana na Rwanda
kuhusu suala hilo kabla ya kuchukua uamuzi huo.
“Ni
uamuzi ambao umeshachukuliwa, hatukushirikishwa kwa namna yoyote na
jukumu letu kama serikali na taifa ni kuwahakikishia ulinzi wote
wanaokuja, na hili ndilo suala tunalolishughulikia kwa sasa,” alisema.
Kwa
mujibu wa gazeti la New Times, Mushikiwabo aliwaeleza waandishi wa
habari kwamba agizo hilo la Rais Kikwete pamoja na ushauri wa kuitaka
Serikali ya Rwanda kuzungumza na wanamgambo hasimu wa FDLR waliopo
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hayatayumbisha uhusiano imara
baina ya Watanzania na Wanyarwanda.
“Sisi si
majirani tu, tuna mfungamano imara baina ya watu wetu pia, tuna
mfungamano wa damu, wa kibiashara, na mengine mengi ya kutufanya
tuendelee kuwa pamoja,” alisema na kutumia fursa hiyo kuwakaribisha
Watanzania nchini Rwanda.
Watanzania
wanaweza kuishi hapa kwa umri wowote wanaotaka. Tunawachukulia kuwa ni
watu wetu muhimu kwenye fungamano la Jumuiya ya Afrika Mashariki,”
alisisitiza.
Rais
Kikwete wakati akihitimisha ziara yake mkoani Kagera alitoa agizo la
kuwataka wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na wahamiaji haramu ama
kuondoka au kuhalalisha ukazi wao, huku akitoa wiki mbili kwa zoezi hilo
kutekelezwa, kabla ya kuanza kwa operesheni ya kuwasaka watu hao.
Kauli
hiyo ilitokana na kushamiri vitendo vya kihalifu katika eneo la Kanda ya
Ziwa, Rais hakutaja jina la nchi ya wahamiaji hao. Kwa ukanda huo
Tanzania inapakana na Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na DRC.
Pia,
Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi alizungumzia
kusikitishwa na kauli za shutuma, kejeli na udhalilishaji zilizotolewa
na Rais Paul Kagame wa Rwanda dhidi yake.
Mvutano
baina ya Rwanda na Tanzania ulianza kuwekwa hadharani Mei mwaka huu,
baada ya Rais Kikwete kuishauri Rwanda kukaa na kuzungumza na FDLR wenye
makao yao DRC, hatua ambayo haikuifurahisha Serikali ya Rwanda.
Wakati
Rwanda ikieleza hayo jana Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alizungumza
na gazeti hili, na kutaka majibu ya kauli hiyo ya Rwanda yatolewe na
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiao wa kimataifa
Msemaji
wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mkumbwa Ally alisema kauli iliyotolewa na
Rais Kikwete ilikuwa ni ushauri, kwamba Rwanda wanaweza kuukubali ama
la.
“Kilichomkasirisha
Rais Kikwete ni lugha za matusi zilizokuwa zikitolewa na viongozi wa
Rwanda, ila kwa hicho walichokisema sidhani kama kitakuwa na tatizo
kwetu,” alisema Mkumb
Alifafanua
kwamba, alipokuwa mkoani Kagera Rais Kikwete hakutoa agizo la
Wanyarwanda kufukuzwa, bali alitoa agizo la kuanza kwa operesheni ya
kuwakamata wahamiaji haramu, wale wanaomiliki silaha kinyume na
taratibu.
“Rais alizungumzia masuala ya jinai ‘Criminal Element’, siyo kuwafukuza Wanyarwanda,” alisisitiza.
Hatutazungumza na FDLR
Waziri
wa Mambo ya Nje, Louise Mushikiwabo, aliendelea kusema sera ya Rwanda
kuhusiana na makundi ya aina hiyo, iko wazi na haitabadilika, kauli
ambayo amekuwa akiirudia kila mara na kuwataka wote wanaofikiria kuhusu
Rwanda kuzungumza na FDLR kwa namna yoyote kusahau wazo hilo.
“Kama
umehusika kwa namna yoyote na maangamizi, wewe utakuwa adui wa kila mtu.
Ni wazi kwamba Wanyarwanda wote watakuwa kwenye majonzi iwapo kwa namna
yoyote kutakuwa na mawasiliano ya FDLR,” alifafanua.
Kundi la
FDLR ambalo ni kifupisho cha Democratic Forces for the Liberation of
Rwanda, linaundwa na watu walioshiriki kwenye mauaji ya kimbari
yaliyowalenga watu wa kabila la Watutsi mwaka 1994, na kusababisha vifo
vya zaidi ya watu 800,000 kwa miezi mitatu.
Kundi
hilo ambalo limeweka makazi yake mashariki mwa DRC, linadaiwa kufanya
mashambulizi kadhaa yakiwamo ya milipuko ya mabomu nchini Rwanda, ambapo
mwezi uliopita shambulio la aina hiyo mjini Kigali lilisababisha vifo
vya watu watatu na kujeruhi watu kadhaa.
Uhusiano wa kihistoria
Familia
za Rwanda zikiwamo zilizoishi Tanzania tangu miaka ya 1950, zimeelezwa
kuwa zimekuwa zikiwasili nchini humo kupitia mpaka wa Rusumo baada ya
agizo la Rais Kikwete kuwataka wawe wameondoka ndani ya wiki mbili,
kabla ya kuanza kwa operesheni rasmi ya kuwaondoa.