Waasi wa M23 Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamesema kuwa watasitisha mapigano, kufuatia makabiliano makali na wanajeshi wa serikali wanaoungwa mkono na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa ikiwemo JWTZ.
Wengi wa wapiganaji wa M23 ni wanajeshi walioasi jeshi la serikali, wengi wao wakiwa wa kibila la Kitutsi sawa na uongozi wa Rwanda.
Serikali ya DRC na Umoja wa Mataifa zimeishutumu serikali ya Rwanda kwa kuwaunga mkono wapiganaji wa kundi hilo la M23, tuhuma ambazo zimekanushwa na utawala wa Kigali.
Bwana Ban, alizungumza na rais Paul Kagame baada ya serikali yake kuishutumu Congo, kwa kufanya shambulio katika ardhi yake makusudi na kumuua mama mmoja na kumjeruhi mtoto wake.
Msaidizi wa katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa, amenukuliwa akiiambia Umoja wa Mataifa kuwa wapiganaji wa kundi la waasi wa M23, wameonekana wakirusha makombora wakilenga Rwanda.
Serikali ya DRC na Umoja wa Mataifa zimeshutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao wa M23, madai ambayo yamepingwa vikali ya utawala wa Kigali.
Wanajeshi wa Congo wakishirikiana na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa, wamekuwa wakifanya mashambulio dhidi ya waasi hao wa M23 karibu na mpaka wa Rwanda, tangu wiki iliyopita.
Waasi walengwa na UN
Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kutunza amani nchini DRC, Monusco, kiliimarishwa zaidi pale wanajeshi elfu tatu zaidi walipotumwa nchini humo kupambana na waasi hao.Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo, amesema mabomu na makombora kumi na tatu yalirushwa katika ardhi yake siku ya Jumatano na mengine kumi siku ya Alhamisi.
Amewashutumu wanajeshi wa DRC kwa kuwalenga raia wake na kusisitiza kuwa kwa sasa wanajiepusha kulipisa kisasi lakini hawatasita kujibu ikiwa uchokozi huo hautakoma.
Msemaji wa jeshi la Congo Kanali Olivier Hamuli ameiambia BBC kuwa jeshi lake haliwezi kurusha makombora kulenga maeneo yanayokaliwa na raia.
''Waasi ndio wanaoweza kufanya kitendo kama hicho, wapiganaji wa M23 na wala sio wanajeshi wake ndio waliokuwa katika eneo ambalo makombora hayo yalirushwa'' Alisema Kanali Hamuli.
Matamshi hayo yaliungwa mkono na msaidizi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Mulet ambaye aliiambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, wanajeshi wake nchini DRC walishuhudia wapiganaji wa M23, wakirusha makombora wakilenga Rwanda na wala sio wanajeshi wa Congo.
Takriban watu laki nane wamekimbia makwaoi nchini Congo tangu waasi hao wa M23 kuanzisha mashambulio katika eneo la Mashariki mwa Congo Aprili mwaka wa 20120.