ATHARI ZA PICHA ZA NUSU UCHI NA TATTOO ZINAZOZAGAA MITANDAONI...!!
Mwezi wa kujistiri kwa wale wenzangu na mie ndiyo huo umeondoka,
hapana shaka kuna wengine wanasoma hapa, huku wakiwa ndani ya yale mambo
yetu. Siyo ishu, kila mtu ana uhuru wa kufanya kile akipendacho. Nchi
yetu inaruhusu kuvaa chochote, ilimradi tu usiende utupu.
Nakumbuka miaka kama mitatu nyuma iliwahi kutokea hoja kuhusu
mavazi, wengi walisema Serikali ilikuwa na mpango wa kupiga marufuku
vimini na nguo za kubana.
Basi bwana siye tunaopenda mambo hayo roho zilikuwa juu, huku
wengine tukitishia hata kuhama nchi ikiwa tutafikia huko kwa kukatazana
mavazi.
Lakini kwa bahati nzuri rais wetu, Jakaya Kikwete alilitolea tamko
suala hilo na kusema kuwa kila mtu ana uhuru wa kuvaa kile
anachojisikia, ili mradi tu asiende utupu. Hapo alimaliza kila kitu.
Tuachane na mambo ya mavazi, suala la msingi leo ni ‘mapicha’ na
tattoo tunazochora mwilini na kuzitupia mtandaoni kila kukicha. Turudi
kulekule kwenye uhuru wa kufanya kile unachojisikia, lakini usiku
ukienda kulala jiulize mwisho wake nini?
Mimi
na wewe hatujui kesho tutakuwa kina nani katika dunia hii, labda
uniambie wewe huna ndoto za kufanya jambo litakalokufanya ukumbukwe,
hata ukitoweka kwenye uso wa dunia.
Kila mtu, hasa wasichana waona fahari kuweka picha za nusu uchi
katika mitandao ya facebook, twitter na sasa instagram . Ujana, maji ya
moto, kwa sasa hizo ‘likes’ na ‘comment’ unazopata zinakuvimbisha
kichwa, lakini naamini baadhi yetu, miaka kumi ijayo tutatamani kurudi
nyuma ili tuondoe historia mbaya tulioiweka mtandaoni.
Picha hizi zitatumika kukugandamiza kwa chochote unachokusudia kukufanya wakati huo. Ni nani atamchagua kiongozi
mwenye picha kama zako unazotupia sasa.Kampuni gani yenye heshima itakayomwajiri mtu mwenye sifa mbaya kwa jamii.
Watu wengi wana uwezo kuona kinachoendelea kwenye mtandao, kumbuka
miaka sita au saba kutoka leo siyo mbali, watu watakumbuka, wengine
watakuwa na picha zako. Wasiokupenda watazitumia kama silaha ya
kukuangamiza.
Kitu kingine ambacho unaweza kuja kukijutia ni hizo tattoo
unazochora hivi sasa. Wapo watu hivi sasa wanalazimika kuvaa mashati
yenye mikono mirefu, suruali au nguo zenye kuficha maeneo fulani ili
waifiche michoro hiyo.
Itafika wakati unashindwa hata namna ya kuwaeleza watoto wako kwa kuwa wengi wanachora kwa kufuata mkumbo au kwa
kuona Rihanna, Chris Brown kachora.
Alafu ubaya wengine huchora majina ya
wapenzi wao tena sehemu ambazo mtu unaweza kujiuliza alichorwaje,mbaya
zaidi ni pale unapochorwa jina la mpenzi wako anaeitwa kwa mfano tuseme
Peter alafu unakuja kuolewa labda na George,hivi unafikiri itakuwaje?
Sawa wanaume wengine wanaweza wasijali sana lakini je wewe utakuwa
unajisikiaje umeolewa na Peter huku umejitattoo George kifuani au
kiunoni na haitoki for the rest of ur life kwasababu huwezi kufuta?...
Ni mtazamo tu...