Friday, July 5, 2013

MWENYEKITI WA CHADEMA AOMBE RADHI KWA HILI

Mwenyekiti wa CDM Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Dr. Wilbrod Slaa wakiteta
Mbowe anatuangusha na anaangusha harakati za kuikataa CCM na serikali yake. Lakini zaidi anatutisha sisi wengine kuhusiana na uwezo wake wa kupima na kutumia hekima kuamua mambo. Lakini zito kabisa ni kuwa anafanya juhudi za kuiondoa CCM madarakani ifikapo 2015 kuwa dhaifu zaidi na hivyo kuongeza ugumu usio wa lazima kwa harakati hizo. Jambo pekee analoweza kufanya ni kusimama na kuomba radhi wanaharakati wenzake ambao wamefanya na kutumia muda mwingi sana kuhakikisha kuwa jamii ya kimataifa inajua kinachoendelea Tanzania wakati wa ziara ya Obama. Baadhi yetu tulitarajia kuwa CDM wangegongelea msumari wa mwisho wakati wa ziara ya Obama.

Niseme kuwa ninachosema hapa hakihusiani na Obama bali uongozi wa Mbowe katika suala la dhifa hii. Sina tatizo na watu wengine kushiriki na kufurahia kuonana na Obama; nina tatizo la msingi na Mwenyekiti wa CDM, chama ambacho sasa hivi kina mgogoro na serikali na ambacho kimekuwa kikinyanyaswa Bungeni na mikoani kuhudhuria hafla ambayo ataonekana kukubali na kubariki serikali. Lakini zaidi kuwa kiongozi huyo kabla ya ujio mzito wa Obama hakutoa kauli yoyote nzito ambayo ingeonesha kutaka vyombo vya habari vya kimataifa na nchi marafiki na watu wengine wajue kinachoendelea nchini dhidi ya upinzani, haki za binadamu na uhuru wa maoni.

Barua ya CPJ na Makalaza za Magazeti ya Marekani
Baadhi ya watu walishangazwa na hata kufurahishwa kwanza kuona Kamati ya Kutetea Waandishi (Committeee for Protection of Journalists) imeandika barua kali kwa Rais Obama kudokeza juu ya kudoda na kudorora kwa tasnia ya uandishi huru wa habari. Barua ile ya CPJ ambayo ilitolewa nakala kwa watu mbalimbali iliweka bayana mifano dhahiri ya jinsi dola inavyotumika kuminya na kudumaza uandishi huru wa habari kiasi kwamba sasa hivi uandishi unaokubalika na kuonekana ni halali ni ule usio kuwa mkali, usiogusa serikali kwa ukali na wale usiowagusa vigogo kwa ukali. Yaani, uandishi wa makala nyororonyororo zilizopakwa mafuta na kupendezeshwa zisizoweza kuudhi hata kulazimisha chombo cha habari kufungiwa.
Mauaji ya Mwandishi wa Habari Daud Mwangosi yaliyofanywa na Polisi kwenye ofisi za CDM Iringa
Kutokana na hali hii mbaya ya uandishi wa habari hali imefika ambapo waandishi na vyombo vya habari vinakuwa compromised japo watawala wataonesha wingi wa vyombo vya habari kuwa ni dalili ya kukomaa kwa haki hii ya msingi ya wananchi.

Hata hivyo barua ya CPJ haikuja hewani hivi hivi tu au kwamba hao watu wa CPJ walikaa NY au Nairobi na wakafikiria tu labda waandike kitu tu kutoka kwenye magazeti. Ukweli ni kuwa CPJ imekuwa ikishirikiana na waandishi mbalimbali wa Kitanzania ndani na nje na kutuma hata watu wake ili kufanya uchunguzi yanapotokea matukio mbalimbali. Kwa wale ambao hawakumbuki mwaka 2008 wakati wa ujio wa Rais Bush (Mwezi Februari) na katikati ya sakata la Richmond Bungeni mtandao uliotangulia huu wa JamboForums ulijikuta kwenye matatizo makubwa baada ya waasisi wake kutiwa mbaroni na polisi kiasi cha kuhusishwa na masuala ya ughaidi. Wengi wanaweza kuwa wamesahau lakini baadhi yetu tunakumbuka kama vile ilikuwa jana kwani tuliweka rehani kila kitu ili kusimama kuwatetea ndugu zetu lakini zaidi sana kutetea haki ya uhuru wa maoni. Kwa wanaokumbuka mimi nilienda BBC Idhaa ya Kiswahili kuzungumzia hili na kutetea uhuru wa mawazo na kusema “hata mawazo ya kijinga yana haki kutolewa”. Lakini hatukuishia hapo, DCI Manumba na IGP Mwema tuliwasumbua kutaka maelezo ya vijana wetu kutiwa mbaroni; hatukujali sana kuwa kuna ugeni mkubwa nchini. Waliachiliwa bila kushtakiwa kwa lolote.
Baada ya Mauaji ya Januari 5, 2011 Arusha yaliyofanywa na vyombo vya dola, Mbowe akiongoza maelfu ya waombolezaji; Kulia Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema

Makala ambazo zimetoka kwenye magazeti ya Washington Post, New York Times na hata USA Today hazikutoka kwa sababu finally vyombo hivi vimeonesha kujali kinachoendelea Tanzania. Kwamba, vyombo hivi vikubwa hatimaye vimeamua kutokana na wema wake kumulika Tanzania. Kufikiri hivyo ni kuwa na mawazo mafupi sana. Kuna watu wanaharakati kwenye media na nje ya media ambao wamejitahidi kuwasiliana na hawa watu na kuwadokeza kwa kina kinachoendelea. Hata swali ambalo Rais Kikwete aliulizwa na mwandishi wa NBC halikutokea peponi; hivi mnafikiria mambo ya Alan Mzengi na kesi yake ilianzia Washington Post? Au NBC? Kuna watu wamejitahidi kumulika ukandamizaji aliofanyiwa dada Yule na zawadi ambayo Alan Mzengi alipewa na Rais Kikwete Ikulu (wenyewe walisema ni Mshauri wa Rais kitu si cha kweli).

Sasa watu wanapofanya haya ili kusaidia harakati za mabadiliko wanatarajia kuwa wale viongozi wa kisiasa na wenyewe wataonesha kuelewa cue za wanaharakati wenzao na kuzitumia vizuri. Sasa watu wakijua kuwa macho ya kimataifa yatakuwa Tanzania na vyombo vya habari vya kimataifa vitakuwa vinaripoti moja kwa moja kutoka Tanzania tulitegemea viongozi wa vyama vya upinzani na hasa CDM wangeonesha kutumia nafasi hii vizuri. Niliandika hili mapema huko nyuma sitalirudia. Badala yake wale wale walioenda kunywa juisi Ikulu, kusifia kazi nzuri ya CCM na serikali yake ndio hao hao tena wameenda kuubariki utawala huu mbele ya jamii ya kimataifa na kupoteza nafasi adhimu waliyopewa na kubebewa na wengine.

Yaani ni kana kwamba watu wametengeneza pasi zote nzuri kuelekea golini na hata pale golini golikipa kapigwa change na sasa ameachiwa mchezaji nyota amalize na badala yake anaunawa mpira na kuupigapiga mabusu! Yaani angalau angefanya kama alivyojaribu Yule Mghana Kombe la Dunia na kupaisha kuliko kushindwa hata kujaribu! Hivi ndivyo alivyofanya Mbowe kwa harakati. Leo hii tunaposikia wana CCM wakiibeza CDM na viongozi wake wanafanya hivyo kwa haki kabisa!

CCM inahangaika kuidhoofisha CDM, CDM inahangaika kuiimarisha CCM? Nimewahi kuandika huko nyuma kuwa si jukumu la upinzani kusaidia chama tawala kutawala. Jukumu la upinzani mahali popote duniani ni kuona chama kilichoko madarakani (siyo serikali tu) kinadhoofika na kushindwa ili hatimaye wananchi waamue kukikataa na kukichagua chama kingine. Hii ndiyo dhana hasa ya upinzani. Wapinzani siyo washauri nasaha wa chama tawala! Kwamba chama tawala kikiwa kwenye matatizo basi upinzani ndio unakataa kusikiliza na kutoa mrejesho na baadaye watawala wanafanya vizuri huku chama cha upinzani kinajisifia ‘tuliwapa sisi ushauri nasaha’! CCM inatambua – na inatambua hili kwa muda sasa – kuwa tishio lake kubwa zaidi ni CDM na hivyo inatumia silaha zote kutoka katika ghala lake kuhakikisha kuwa CDM inadhoofika na kuporomoka. Nahitaji kweli kutoa mifano juu ya hili? Kesi za kila aina dhidi ya viongozi wa upinzani, tuhuma za ughaidi, na kunyimwa vibali vya kila namna tunaweza kusema CCM inaipenda saaaaana CDM kiasi cha kumwalika mwenyekiti wake (nafahamu mwaliko umetoka ‘serikalini’). Leo hii kuna tuhuma za kila namna jinsi viongozi wa CCM wanavyowasiliana sana na watu wa serikalini ili kuidhibiti CDM. Sasa tuseme Mbowe yeye halioni hili au halioni kwa uzito wake?
]Viongozi wa CDM wakifikishwa mahakamani Arusha; katikati ya Mbowe na Dr. Slaa ni Mbunge wa Moshi Mjini Philemon Ndesamburo


Niliandika huko nyuma kuwa siwalaumu kabisa CCM kujaribu kudhoofisha upinzani nchini – hilo ndilo jukumu la chama tawala. Jukumu la chama tawala kwa upinzani ni kuudhofisha ili usije kupata nguvu ya kukiondoa madarakani. Ni rahisi hivyo. CCM haifanyi jambo lolote lisilo la kawaida (atypical) la vyama vya siasa vilivyoko madarakani mahali popote. Hivi, si serikali ya Obama hapa imejikuta na kashfa ya IRS na kashfa ya ushushu? Hiyo ya IRS si imedaiwa kuwa IRS (Internal Revenus Service) imekuwa ikivifuatilia kwa karibu zaidi vikundi vya kihafidhina kuliko vile vya kiliberali? Sasa inashangaza?

Kauli za Mbowe zinatatiza harakati
Alipoamua kusifia serikali ya Kikwete wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Kwa Sadala Mbowe alinukuliwa kusema: “Mimi ni mpinzani na Mheshimiwa Rais unajua hilo, lakini wanasema ‘mnyonge mnyongeni haki yake mpeni’. NInatembea sana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa barabara na kwa anga; na mheshimiwa Rais tunakupongeza na mheshimiwa Waziri tunakupongeza kwa kazi kubwa sana ya kujenga miundombinu inayofanywa ndani ya taifa letu”


Kauli hii kwa kuiangalia kwa haraka haina tatizo lolote lile na kwa kweli mtu atasema kuwa Mbowe alistahili kuitoa. Hata hivyo, bahati mbaya sana imetolewa na kufanya watu wasahau kiasi cha changamoto kilivyo. Lakini zaidi ni kusahau kuwa karibu kwenye majimbo ambayo CCM imekuwa ikipata shida ndiko ambako pia CCM na serikali yake iko kwenye charm offensive.
Mbowe akiinama kutoa pongezi kwa Rais Kikwete na serikali yake kwa kuwapa miundo mbinu Oktoba 2012
Mbowe kama kiongozi wa upinzani – na mwenyewe alisema anajijua hivyo – jukumu lake siyo kumwaga sifa. Kama kweli Mbowe anaamini CCM na serikali yak echini ya Kikwete inafanya kazi nzuri sana ya kujenga miundo mbinu mbalimbali atapaswa kutuambia kwanini bado watu waitoe serikali hii madarakani? Kwanini wawaondoe CCM kama wanafanya kazi nzuri sana hivyo na hasa eneo la miundombinu ambalo lina mahitaji makubwa sana. Kushindwa kuonesha kuwa kilichofanywa ni kiduchu kulinganishwa na kilichoahidiwa ni kosa kubwa la mkakati; lakini pia kushindwa kuonesha suala la ubora wa miundo mbinu na rushwa iliyioko katika ujenzi na ufisadi ni kosa jingine. Ni kana kwamba kwa vile kunakojengwa ni kwao basi kafumbia matatizo kabisa yanayoendelea nchini. Hili lilikuwa kosa ambalo angetakiwa kuomba radhi wakati ule.

La kukubali mwaliko wa dhifa ni kosa kubwa zaidi Sasa hilo la kumsifia Kikwete tunaweza kuliweka pembeni na kusema kuwa alikuwa mbele ya Mangi na yeye alitaka kuchomekea mambo mawili matatu. Hili la Obama hata hivyo ni la makosa makubwa ya kimkakati (strategic errors) kiasi kwamba nashindwa kuelewa kama wanazungumza na wapanga mikakati wao au kila mmoja anajiendea kivyake vyake.
Kikwete na Obama kwenye dhifa ya kitaifa
Masaa machache kabla ya habari kuwa Mbowe amekubali mwaliko na amehudhuria dhifa ya Obama Katibu Mkuu wa CDM Dk. Slaa akinukuliwa na gazeti la Mwananchi alinukuliwa kusema kuwa chama chake hakikupokea mwaliko wowote wa kuhudhuria mapokezi ya Obama na hivyo wasingeenda kule. Katibu Mkuu ndiye mtendaji Mkuu na barua za Mwaliko bila ya shaka zinaandikwa kwenda kwake. Hivyo, wengi tulijua kuwa kama hawajapata mwaliko basi hawaendi; siyo kususa! Unasusa pale ambapo umepata mwaliko na unaamua huendi.

Swali kubwa ambalo baadhi ya watu wameuliza na Mbowe atapaswa kulitolea majibu wakati wa kuomba radhi ni kuwa alipopata mwaliko wa kwenda kula ‘dina’ Ikulu alikuwa aliwasilina na Katibu Mkuu wake? Na je alijua kuwa Katibu wake alitangaza kuwa hawakualikwa? Lakini nyuma ya hilo swali jingine labda ni la haki zaidi ni kuwa Mbowe alipata mwaliko wa dhifa lini? Kama aliupata mapema zaidi kabla ya Dr. Slaa kuzungumza na mwananchi linaacha maswali mengine; kama aliupata masaa machache kabla ya tukio lenyewe nay eye alikubali nalo linaacha maswali mengi zaidi.

Tatizo la Msingi basi ni nini? Kwa maneno machache ni kuwa kuna mgogoro kati ya CCM na serikali yake na CDM. Kumekuwepo na matukio mengi yanayoonesha unyanyasaji na ukandamizaji wa wapinzani nchini, matukio ambayo nikijaribu kuyaorodhesha hapa itakuwa ni kurudia rudia wimbo ule ule kwa wanakwaya! Matukio haya yameonesha wazi kabisa kuwa kuna uhasama wa kisiasa (political animosity) kati ya CCM na CDM. Hali ambayo haijatengemaa na kama matukio ya Arusha ni ushahidi hakuna dalili ya kutengemaa. Kesi mbalimbali ambazo zimekuwa zikifunguliwa, vitisho na unyanyasaji wa viongozi wa CDM ni sehemu tu ya mkakati huo wa kuidhoofisha CDM. Mbowe mwenyewe ameshasema mara nyingi kwenye mikutano jinsi CCM na serikali yake na vyombo vya dola vinavyowanyanyasa.
Sasa, ama Mbowe anasema kweli kuhusu vitendo vya CCM na serikali dhidi ya CDM au vitendo hivyo si vibaya kihivyo. Kama anasema kweli – na ninaamini hivyo – ni jukumu lake kuhakikisha kuwa siyo tu Watanzania wanajua hili (kwani tayari wengi wanalijua) bali jamii ya kimataifa inajua hili vile vile. Katika kuijulisha jamii ya kimataifa hakukuwa na nafasi nzuri zaidi ya kufanya hivyo kaa ujio wa Obama.

Wengine wanasema alialikwa siyo kama Mwenyekiti wa CDM bali kwa sababu ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni (KUB); really? Na watu wenye kusema hivi wanazungumza kabisa kama wana hekima? Kiongozi wa Upinzani wa chama gani huko Bungeni? Na hivi huko Bungeni kuna mahusiano mazuri sana baina ya CCM na CDM kiasi kwamba Mwenyekiti wa CCM akiandaa kitu basi KUB ni lazima aende kwa vile kaalikwa? Hivi siyo ndio huko Bungeni ambako tumeona mojawapo ya unyanyasaji mkubwa zaidi wa CDM? Mbowe anayaona au pia haoni?

Kama Shida ilikuwa ni kupeana mkono na Obama Sasa inawezekana Mbowe kama wengine wengi walitaka na kuwa na hamu ya kupeana mkono na Rais wa Marekani; tena Mweusi “mwenzetu” angalau na wao wawe na la kusema kuwa tulipeana mkono na Obama au kula naye meza moja. Hii kweli yaweza kuwa sababu ya kutosha kuvunja kanuni zote za kupigania haki na kukipaisha chama mbele ya jamii ya kimataifa? Hivi, keshokutwa serikali hii hii ikimtia pingu tena au ikiwanyanyasa tena kwenye mikutano kwa kukataa “kutii bila shurti” Mbowe atasimama na kutaja jina la Kikwete na Serikali kuwa wana matatizo? Really?


Mtu anaweza kusema ati ujio wa Obama ni suala la kitaifa na halihitaji siasa? Oh yeah? Hivi CCM na wanachama wake wakianza kujitamba kuwa Mwenyekiti wao ndani ya uongozi wake ameweza kuwaleta viongozi mbalimbali wa kimataifa na kupata misaada bwelele watakuwa na makosa; kwamba na wapinzani nao waliomba sana wawekwe kwenye ratiba kuna watu watabisha? CCM wana haki zote za kutumia ziara hizi zote kwa kampeni zao; zinajenga chama na utawala wao madarakani. Sasa kiongozi mkuu wa upinzani anapobariki anajidhoofisha na kudhoofisha upinzani!

Kama kweli walikuwa wanataka kukutana na Obama Mbowe na wenzake wajitahidi kuiondoa CCM madarakani 2015; kwani Obama bado atakuwa na mwaka mmoja madarakani! Ama wamekata tamaa ya CCM kuondoka madarakani.

Mbowe Aombe Radhi Ninachopendekeza ni kuwa Mbowe aombe radhi wanachama wake, mashabiki wake na wengine ambao wamekwaza na kitendo chake hiki; lakini vile vile aoneshe kuwa anatambua kinachogombaniwa ni kikubwa zaidi kuliko kujisogeza kwa watawala. Tayari tumeona kujisogeza kwao wakati wa kwenda Ikulu suala la Katiba Mpya hakukuwasaidia; kujisogeza kwao na kelele zao zilizuia vipi Kamuhanda kupandishwa cheo? Si Kikwete huyu huyu amempa IGP Mwema Nishani ya Utumishi Uliotukuka? Halafu kiongozi wa CDM anaenda na kuonesha “umoja” na wakandamizaji wake? Hivi kesho kutwa RPC wa Arusha ambaye amekuwa akimnyanyasa Lema au Mkuu wa Mkoa akipewa vyeo zaidi na Kikwete Mbowe atasema neno?
Mbowe kama Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini anapaswa kuchora mstari ambao yeye mwenyewe hatouvuka. Watu wanataka kuona tunaelewa nani yuko upande gani? Hivi, Mbowe kwa ukaribu wote na Kikwete mbona Kikwete hadi leo hajaunda tume hata moja ya Kimahakama? Halafu anamwalika Ikulu anakwenda?

Mbowe aombe radhi kwa uamuzi wake huu; lakini kama anaona hawezi na kuwa anataka kuendelea kuwa karibu na Kikwete na serikali yake atafanya jambo jema sana kuachia ngazi uongozi ili CDM ipate uongozi mwingine ambao utajua na kusimamia kile inachopigania. Hata kama kwa kufanya hivyo wataonekana hawaoneshi umoja, heshima, na utaifa mbele ya wageni. Wakati mwingine mambo mengine yanahitaji kukataliwa tu na kupingwa.

Jambo pekee ambalo watu huja pamoja bila kujali itikadi, siasa na hata mambo mengine ni misiba tu. Na hata hapo kuna mistari mingine haivukwi.
Mimi Mwanakijiji