Wednesday, July 17, 2013

MSIBA MWINGINE TENA GHAFLA

MWENYEKITI WA HALMASHAURI AFARIKI DUNIA BAADA YA KUANGUKA CHOONI

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Laurent Hoya, amefariki dunia ghafla jana alfajiri baada ya kuanguka chooni. Kifo hicho kimetokea nyumbani kwa marehemu Nkuhungu katika Manispaa ya Dodoma.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Fatma Ally alisema Hoya ambaye alikuwa na tatizo la ugonjwa wa moyo, alianguka chooni jana alfajiri na kukutwa na mauti.


“Tuliachana juzi saa 7.30 mara baada ya kikao, taarifa ya kifo chake nilizipata saa 11 alfajiri jana, ni kifo cha ghafla sana na halmashauri imempoteza mtu ambaye alikuwa mfano kwa jamii,” alisema.


Hoya ambaye alikuwa Diwani wa Kata ya Mpwayungu, anatarajiwa kuzikwa kijijini kwake Mpwayungu kesho.


Mkuu huyo wa Wilaya alisema alikuwa akishirikiana kwa karibu na Mwenyekiti huyo, kwani alikuwa kiongozi mwenye ushirikiano mkubwa na hakuwa mtu wa kukwepa kuitikia mwito.

Alisema alikuwa akilima mazao yanayohimizwa katika mkoa wa Dodoma na shamba lake mwaka huu lilikuwa la mfano, kutokana na kulima ekari 300 za mtama na kusaidia wakulima mbegu kwa ajili ya kilimo cha zao hilo.