Ndege ya kivita F-16
Marekani inaendelea na mpango wake wa kutoa ndege za
kivita kwa jeshi la Misri licha ya msukosuko wa kisiasa unaokumba nchi
hiyo. Hatua hii inajiri wakati Marekani ikiendelea kutathmini matukio ya
wiki jana ambapo jeshi lilimuondoa madarakani Rais Mohammed Morsi.
Msaada wa kijeshi kwa Misri ungesitishwa endapo
Marekani ingelitaja matukio ya wiki jana kama mapinduzi ya kijeshi.
Kundi la Muslim Brotherhood linalomuunga mkono Morsi linasisitiza
arejeshwe madarakani.
Wafuasi wake wamekua wakiandamana
karibu na kambi kuu ya jeshi ambapo anaaminika kuuzuiliwa. Hapo
Jumatatu,wafuasi wa Brotherhood 51 waliuawa kwa kupigwa risasi na jeshi
wakati wanakabiliano.
Utawala wa mpito umesema kwamba Bw. Morsi
anazuiliwa eneo salama na kwamba haki zake zinazingatiwa. Maafisa wa
Marekani wamesema ndege mpya za kivita aina ya F-16 zitawasilishwa
katika wiki chache zijazo.
Mpango wa kufadhili jeshi ulianza kutekelezwa
mapema mwaka huu na jeshi linatarajia kupokea ndege 20 za kivita. Msemaji
wa ikulu ya Rais amesema Marekani haitabadilisha mpango wa kufadhili
jeshi la Misri, japo inaendelea kutathmini kuhusu matukio ya kisiasa.
Msaada wa kijeshi nchini Misri ambao hutolewa na Marekani hufikia dola
bilioni 1.3 kila mwaka.
Hapo Jumanne, kibali cha kumkamata kiongozi wa
Muslim Brotherhood Mohamed Badie kilitolewa pamoja na wakuu wengine tisa
wa kundi hilo. Viongiozi hao wamelaumiwa kwa kuchochea ghasia mjini
Cairo ambapo zaidi ya watu 50 waliuawa na mamia kujeruhiwa.