WIZARA ya
Afya na Ustawi wa Jamii, imeanza kuwaajiri madaktari waliokuwa
wamefukuzwa kazi wakati wa mgomo uliotokea Oktoba mwaka juzi. Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa wizara
hiyo, Nsachris Mwamwaja, alisema hatua hiyo imechukuliwa ili kuondoa
uhaba wa madaktari nchini. Mwamwaja
alisema kuwa wizara imefanya mabadiliko katika mwaka wa fedha wa
2012/2013, baada ya kupata kibali cha kuwapangia vituo vya kazi
wataalamu wa afya 8,869.Madaktari
hao wanapelekwa katika mamlaka mbalimbali ikiwemo hospitali za
mashirika, tawala za mikoa, Taasisi ya Saratani Ocean Road, Hospitali ya
Rufaa ya Bugando na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mwamaja
alisema hadi kufikia sasa wizara imejitahidi kupunguza upungufu wa
watumishi wa afya, ambapo asilimia 53 ya watumishi wapo kazini, huku
wizara ikiwa na changamoto ya upungufu wa watumishi wa afya kwa asilimia
47.
“Jitihada hizi za kuongeza watumishi wa afya itasaidia kupunguza
madaktari wanao kwenda kusoma nje ya nchi, kwani madaktari watakuwa ni
wengi ukilinganisha na miaka ya nyuma.
“Tuna mpango wa kujenga nyumba za wafanyakazi na kununua vifaa vya afya
ili kuboresha afya ya wananchi ambapo madaktari 1,077 wapo katika vituo
vya kazi ukilinganisha na miaka ya nyuma hapakuwepo na ajira za
kutosha,” alisema.
Sanjari na hapo alisema kuwa Serikali imeendelea kuongeza udahili katika
vyuo vyake, ambapo mwaka 2009/2010 wanafunzi 5,365, walidahiliwa na
mwaka 2010/2011 wanafunzi 6,713,2011 walidahiliwa.