Thursday, June 13, 2013

YOUNG AFRICA HAITASHIRIKI MASHINDANO YA VILABU BINGWA AFRIKA MASHARIKI NA KATI

Mabingwa watetezi wa  Kombe la Kagame kwa miaka miwili mfululizo timu ya Young Africans hawatashiriki tena mashindano ya Vilabu Bingwa Afrika Mashariki Kati  (CECAFA Kagame Cup) yaliyopangwa kuanza kutimua vumbi nchini Sudan wiki ijayo Juni 18 siku ya jumanne.
Young Africans haitashiriki mashindano hayo kufuatia kauli ya serikali ya juu ya kutozirushu timu zake kwenda kwenye mashindano hayo kutokana na hofu ya usalama kwa wachezaji na viongozi wakati wa mashindano hayo.
Mapema jana Bungeni Naibu Waziri wa michezo na Utamaduni mh Amos Makalla alisema hali ya usalama katika miji ya El- Fashir na Kadugli sio nzuri, hivyo wao kama serikali hawataziruhusu timu za kutoka Tanzania kwenda kushiriki michuano hiyo kutokana na hali ya usalama kwenye majimbo hayo.
"Sehemu ambayo mashindano yanafanyika hakuna usalama wa kutosha, mwisho kutembea saa 12 jioni, huduma za hoteli ni duni hazijitoshelezi kuweza kukaa kwa timu katika miji hiyo na kubwa zaidi ni hali ya usalama, kutoka Khartoum mpaka Al Fashir inabidi kutumia usafiri wa Helikopta kitu ambacho bado ni hatari" alisema Makalla"
Kufuatia kauli hiyo ya waziri mwenye dhamana ya michezo timu ya Yanga haitashiriki mashindano hayo, Yanga inajiondoa kwenye mashindano hayo moja kwa moja kufuatia kauli hiyo ya serikali ya kuzizuia timu za Tanzania kutoshiriki michuani hiyo kutokana na hofu ya usalama kwa raia wake.
Kocha mkuu Brandts mara baada ya taarifa hiyo ya serikali amesema ni jambo la busara, serikali imetazama mbali na kuona umuhimu wa usalama kwa watu wake, kwani hamuwezi kucheza michuano zaidi wa wiki mbili katika maeneo yanayolindwa na vikosi vya jeshi vya kutuliza amani kutoka sehemu mbali mbali.
Yanga iliyokua imeanza mazoezi wiki iliyopita kujiandaa na mashindano hayo, kwa sasa itakua na mapumziko ya wiki mbili kabla ya kuanza tena mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom.