Friday, June 14, 2013

OMMY DIMPOZ AMTUKANA MAREHEM NGWAIR MATUSI YA AJABU

AFUNGUKA VIBAYA KUWA HAWEZI KUFA MASIKINI KAMA NGWEA NA AMECHOKA KUZIKA MASIKINI

MSANII OMMY DIMPOZ AKOSA HESHIMA ,,,, asiye na adabu hakosi sababu ya kuharibu, mwenye mdomo mchafu ni ada yake kutoa neno chafu, mwanamuziki chipukizi, Omar Faraji Nyembo ‘Ommy Dimpoz’, amedhihirisha kuwa ana kiwango cha juu sana cha dharau kwa kumdhihaki na kumtusi mtu aliyetangulia mbele za haki.
Utamaduni wetu Tanzania na kama ilivyo kwa mafundisho ya dini kupitia vitabu vinne vitakatifu, Torati, Zaburi, Injili na Kuran, fundisho ni kwamba mja aliyepoteza maisha hakashifiwi, hasimangwi, hahukumiwi, isipokuwa huhifadhiwa kwa heshima kisha kuombewa salama na amani mbele ya Mungu.

Ommy Dimpoz, kijana ambaye ni mwaka jana tu alikuwa ‘anawanga’ huku na huko mikono nyuma akiomba msaada wa kimuziki, hivi sasa anajiona ameota meno ya juu kuweza kung’ata, kiburi hicho kimempa uthubutu wa kumtusi Mfalme wa Freestyle, marehemu Albert Kenneth Mangwea ‘Ngwair’.

Thamani ya Ngwair na namna alivyozikwa kwa heshima hajaviona, badala yake akatusi kuwa Mfalme wa Freestyle alikufa maskini ndiyo maana mazishi yake yalikuwa ya kuungaunga michango ya wadau.


Kifo cha Ngwair, kilivuta makundi mbalimbali kushiriki kwa hali na mali kuchangia na kumzika, taifa lilizizima mkoa kwa mkoa, mguso huo wa kitaifa aliokuwa nao mwanamuziki huyo, Ommy hakuuona, isipokuwa akanena: “Sitaki kufa maskini kama Ngwair.”
Marehemu Albert Kenneth Mangwea ‘Ngwair’.

Akimweleza mwandishi wetu kwa nyakati tofauti, Juni 10 (Jumatatu) na Juni 11, mwaka huu (Jumanne), Ommy alidhihaki hata ushiriki wa wanamuziki waliosimamisha shughuli zao kwa muda kisha kuungana na kushikamana kuhakikisha Ngwair anazikwa kwa heshima.
 
“Sitaki nikifa yatokee kama ya Ngwair, amekufa Afrika Kusini, hata kuusafirisha mwili kuuleta Tanzania imebidi mpaka watu wachangie, ile ni aibu sana,” alisema Ommy kwa dharau.

Kutokana na uzito wa maneno ambayo Ommy aliyatamka kuhusu Ngwair, siku iliyofuata (Jumanne), mwandishi wetu alimpigia simu kumuuliza kama maelezo hayo ya kashfa aliyatoa akiwa amelewa au la?

Ommy kwa kujiamini, alijibu kwamba alichokisema kuhusu Ngwair ni ukweli kwa asilimia 100.

MWANDISHI: Nakushauri kama mdogo wangu, siku nyingine usirudie kutamka maneno hayo ni mabaya sana kwa mtu aliyekufa.

OMMY: Sijaongea neno baya, nimesema ukweli wasanii hatutakiwi kufa maskini.

MWANDISHI: Wewe unaona mtu akichangiwa baada ya kufa ndiyo kipimo cha umaskini?

OMMY: Kuna mambo mengi ambayo yangefanyika kabla ya kuchangiwa lakini Ngwair alishindwa kuyafanya.

MWANDISHI: Sasa Ngwair angefanya nini wakati yeye ameshakufa?

OMMY: Kuna mambo yangefanyika, mfano kusafirisha mwili kutoka Afrika Kusini.

MWANDISHI: Sasa Ngwair angejisafirisha mwenyewe?

OMMY: Nachosema mimi ni kwamba wasanii hatutakiwi kufa maskini.

MWANDISHI: Sikiliza Ommy, hata mabilionea wakubwa huwa wanachangiwa. Mtu kuchangiwa siyo kashfa wala aibu kama unavyotaka kulionesha tukio la Ngwair. Marehemu Steven Kanumba alikuwa anatembelea Toyota Lexus V8, mbona alipokufa kila kitu alifanyiwa? Ni jambo la kawaida.
 
OMMY: Ngwair alikuwa na ‘stresi’ za maisha ndiyo maana alikuwa anakula unga.
 
MWANDISHI: Ulishawahi kumwona Ngwair akitumia unga?
 
OMMY: Kwanza nakusikia unanirekodi, sijui una malengo gani.
MANENO YA KASHFA MLIMANI CITY
Juni 8, mwaka huu, katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, wakati wa utoaji wa Tuzo za Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA)  mwaka 2012-2013, Ommy Dimpoz alizungumza maneno ya kashfa ambayo moja kwa moja yalitafsiriwa ni dongo kwa Ngwair.
 
Baada ya kutangazwa mshindi wa kipengele cha Video Bora ya Mwaka na kukabidhiwa tuzo yake, Ommy alibwabwaja: “Jamani tumechoka kuzika wasanii maskini wenye majina makubwa.”
Japo hakutaja jina la yule aliyekuwa anamzungumzia, tafsiri ya wengi ni kwamba Ommy alikuwa anamzungumzia Ngwair kwa sababu ndiye staa aliyekuwa amezikwa kishindo cha siku moja tu kabla ya usiku huo wa tuzo. Ngwair alizikwa Alhamisi, tuzo Jumamosi.
 
“Huyu dogo ana nyodo sana, sasa haya ni maneno gani ya kuzungumza? Hapa anamzungumzia Ngwair, ila anapaswa kujua kwamba yeye bado msanii mdogo sana kumlinganisha na Ngwair,” alisema mtangazaji mmoja kwa masikitiko.