
Baada ya kutoka sare jana na Mtibwa Sugar katika mfululizo wa raundi ya michuano ya ligi kuu ya Vodacom, klabu ya Simba imelalamikia ratiba ngumu iliyopangiwa na shirikisho la soka nchini TFF – wakicheza mechi 3 ndani ya siku 11 huku wakitakiwa kwenda na kurudi Mbeya bila sababu.
Simba ambayo jana ilitoka sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar katika dimba la
Jamhuri Morogoro, itasafiri hadi Tanga kucheza na Mgambo JKT Jumapili
halafu itaenda Mbeya kuivaa Mbeya City Februari 15.
Simba itarejea Dar es Salaam kucheza michezo miwili dhidi ya JKT Ruvu
(Februari 23) na Ruvu Shooting (Machi 2) halafu itaenda Mbeya tena
kucheza na Prisons (Machi 8).
Akizungumza na gazeti la Mwanaspoti, kocha msaidizi
wa Simba, Seleman Matola alisema: “Kwanza hizi mechi zote ni ngumu,
halafu zinachezwa kwa ukaribu, tutakuwa na muda mdogo wa kurekebisha
makosa yetu kutoka mechi moja hadi nyingine hivyo lazima tujitahidi sana
kujituma.
“Lakini ukiachana na hilo, tazama zilivyo karibu, hakuna muda wa
kutosha wa kupumzika ukizingatia kila mechi unahama kutoka mkoa mmoja
hadi mwingine, mbaya zaidi tuna kazi ya kwenda Mbeya halafu tunarudi Dar
es Salaam kisha tunageuza kurudi Mbeya tena.”
Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), limetamka kwamba ratiba hiyo imepangwa siku nyingi na ilizingatia mambo mengi.