Kufungiwa kwa Magazeti ya Mwananchi na Mtanzania: tujifunze nini?
Imeandikwa na Dkt. Hamisi Kigwangalla, MB.
Hivi majuzi Ndg. Assah Mwambene ambaye ni msemaji mkuu wa serikali na
mkurugenzi wa idara ya habari maelezo alitoa tamko ambalo lilibainisha
taarifa za kufungiwa kwa magazeti mawili kwa makosa ya uchochezi.
Magazeti haya ni lile la Mwananchi, lililofungiwa kwa siku 14 na la
Mtanzania lililofungiwa kwa siku 90. Yote haya ni magazeti makongwe na
hivyo yanasomwa na watu wengi. Mimi binafsi kwa mfano, kama nitanunua
gazeti moja kwa siku, basi kama siyo The Guardian basi ni lazima
litakuwa ni ‘Mwananchi.’ Kufungiwa kwa magazeti kunayakosesha makampuni
yanayoyamiliki mapato na pia yanawakosesha wasomaji taarifa. Wapigania
haki za binadamu watasema hapa kuwa kuyafungia magazeti ni kuvunja
misingi ya haki za binadamu za kupata taarifa na pia ni kuminya uhuru wa
kupashana habari.
Tayari kuna hoja mtaani kwamba sheria ya magazeti ya mwaka 1976
iliyotumika kutoa habari hizi ni ya ‘kizamani’, ‘imepitwa na wakati’ na
ingepaswa kufutwa. Kuna hoja nyingine kwamba sheria hiyo ina vifungu 18
vinavyokwenda kinyume na misingi ya haki na uhuru wa kupashana habari,
ambao kimsingi unalindwa na katiba. Rafiki yangu Mhe. Zitto Kabwe (Mb.)
ameiita sheria hii ‘ya kidikteta’ katika makala yake yenye kichwa cha
habari ‘Kufungiwa magazeti – wahafidhina sasa wanaongoza’, na hapa
namnukuu, ‘sheria ya kidikteta ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo tume ya
Jaji Francis Nyalali iliiorodhesha kama sheria kandamizi.’ Mwandishi
nguli wa habari na vitabu, Mzee Ndimara Tegambwage wakati MwanaHALISI
lilipofungiwa mwaka jana aliwahi kuiita sheria hii kuwa ni ‘Draconian’
akiilinganisha na sheria zilizokuwa zikitungwa na mtunga sheria wa
Ugiriki ya kale aliyeitwa Draco, kwa ukali na ‘ukatili’ wake. Haya ni
maneno na mtazamo mkali sana dhidi ya sheria hii. Je, ulazima wa
serikali kuleta mapendekezo ya sheria mpya bungeni? Ama wabunge tuibuke
na kuleta miswada yetu binafsi? Ni maswali yanayohitaji majibu.
kwa vyovyote vile sheria hii ni lazima inahitaji kufanyiwa marekebisho
makubwa ama hata kufutwa na kutungwa sheria mpya itakayoendana na
mabadiliko makubwa ya katiba yaliyopita hapo katikati hususan yale ya
mwaka 1984 yaliyoongeza vipengele vya haki za binadamu (bills of rights)
na yale ya miaka ya ’90.
Katika makala ya Mhe. Zitto Kabwe amekumbushia kauli ya Mhe. Dkt.
Jakaya Kikwete, Rais, kuwa ‘kuna watu wanauchukulia uvumilivu wangu huu
kama udhaifu…..nataka kutoa mfano tu kuwa tuvumiliane’ na pia anatoa
maelezo ya kumnukuu Rais kuwa aliwahi kusema wenzake wanamtaka ‘aongeze
ukali’. Nafahamu nia ya mtu makini kama Rais Kikwete kwenye nafasi ya
uongozi wa juu kama huu alionao ni wazi kabisa itakuwa ni kutaka kuacha
jina lake likikumbukwa kwa mazuri (legacy) na watanzania wenzake. Niweke
kumbukumbu wazi kabisa hapa kwamba hakujatokea Rais aliyeruhusu uhuru
wa vyombo vya habari kama huyu toka taifa hili lizaliwe. Lakini pia
tumeshuhudia hakujatokea bunge lenye wabunge wanaoweza kumtukana Rais
kwa ‘uvumilivu’ wake kama hili. Tulisikia namna Mhe. John Mnyika (Mb.)
wa Ubungo alivyoamua kumtukana Rais bungeni bila sababu na kwa jeuri na
ufedhuli wa hali ya juu. Kwanza Rais ni mzazi kwa Mhe. Mnyika na zaidi
ni kiongozi anayeheshimika kwa mamlaka na nafasi yake kwa taifa letu,
lakini katika hali ya kushangaza watanzania wengi walishuhudia Mhe. John
Mnyika akimwita Rais ‘names’….’akim-label’ ‘dhaifu’ kwa huo ‘uvumilivu’
wake. Vyombo vya habari viliandika jambo hili vikimpamba kuwa ni
mwanasiasa ‘mahiri’ na ‘jasiri’. Hakuna chombo kilichokumbuka kuwa Rais
Kikwete ameamua kuvumilia matusi yale tu. Wala hakuna chombo
kilichomkanya huyu kijana mdogo tu Mhe. Mnyika kwa kumtusi Rais wetu
sote!
Tukio hili lilipaswa litukumbushe kuwa hakuna uhuru usio na mipaka.
Pia hakuna haki isiyo na wajibu. Binafsi suing mkono mkono wa chuma wa
serikali kuiangukia tasnia ya habari nchini, hapana! Pia suing mkono
mambo mengi yanayoandikwa kwenye vyombo vya habari kwa sababu za chuki
binafsi za wenye vyombo hivyo ama wenye mamlaka ya kuahariri habari hizo
ama waandishi wenye maslahi yao binafsi. Wasomi na wana habari kwenye
nchi yoyote ile yenye watu wanaojitambua ndiyo mihimili inayoheshimika
kwa kuwa na utaifa zaidi kwenye maoni yake kwenye mambo mbalimbali
mazito ya kitaifa. Kuwa na maadili ya kazi ni jambo la mbele kabisa.
Husani ukiwa unafanya kazi nyeti kama ya habari ama ya kufundisha
watoto. Kwa sababu unakuwa na jukumu la kimaadili la kuhakikisha
unalinda misingi ya taifa na tunu zake kama amani, upendo, udugu, usawa,
uzalendo, utangamano wa kitaifa, umoja na mshikamano. Kuna mambo
yasiyofaa kushabikiwa (kuwa glorified) na magazeti kwa mfano – uasi kwa
serikali, kuanguka kwa dola, wasiwasi kwa usalama wa Taifa, jeshi la
wananchi na majeshi yetu yote mengine na utengano wenye misingi ya
ukanda, ukabila ama udini. Haya ni mambo ya hatari. Leo hii mtu
akitukana bungeni, na haswa akiwa anaitukana serikali ataandikwa ukurasa
wa mbele na baadhi ya vyombo vya habari kuwa yeye ni shujaa – kwamba
hilo ndilo jambo la kuwaambia watanzania, lakini mwingine atakayechangia
hoja ya kukuza uchumi wetu kupitia kilimo habari yake si mali kitu.
Vyombo vya habari ni taasisi nyeti sana kwenye taifa lolote lile.
Vinaweza kujenga ama kubomoa. Wengine wanapenda kusema ni ‘mhimili wan
ne wa dola.’ Vina kila sababu na ulazima wa kujijenga katika hadhi na
heshima hiyo ya kuwa mhimili wan ne wa dola. Vinatakiwa vifahamu kuwa
jukumu la kujenga taasisi yao ni la kwao wenyewe na heshima haiji bure,
inakuja kwa kujiheshimu pia. Taasisi inapaswa kujenga taswira yake
yenyewe kabla haijaanza kulia lia ijengewe na mtu mwingine. Kuna baadhi
ya vyombo vya habari na baadhi ya wanahabari wamejishusha kiasi cha
kujikuta wameingia kwenye mifuko ya watu ama vingine vinafanya kazi ya
vyama ama wafadhili fulani. Hauwezi kujenga heshima yako kama unashindwa
kusimamia misingi ya kimaadili midogo midogo kama hii.
Kwa vyovyote vile tunahitaji sheria mpya, ambayo tutaijadili na
kukubaliana sote kwamba tunataka sheria mpya iwe na mambo gani, mfano
adhabu zipi ziwekwe kwa yale magazeti yatakayokwenda kinyume na maadili
kama vile kusingizia watu mambo ambayo hawakuyafanya kwa kisingizio kuwa
‘eti ni mambo yanayosemwa semwa mtaani’. Kwamba mwandishi anaandika
akionesha kuwa hata yeye amesikia na hivyo anaandika hivyo hivyo kwa
kusikia sikia kwake. Anajua kabisa akienda mahakamani hatofungwa na
sheria kwa sababu hakusema ‘moja kwa moja’ kuwa Fulani amefanya nini
bali alisema habari ya kusikia sikia tu! Sasa tunataka sheria mpya
itungwe na iweke bayana adhabu zitakazochukuliwa dhidi ya magazeti
yatakayokuwa yakifanya utumbo unaofanana na huu. Mimi si mshabiki wa
Sheria yoyote ile kandamizi lakini ni muumini mkubwa sana wa
uwajibikaji. Atakayekosa basi na apewe adhabu stahiki yake kulingana na
kosa lake. Mfano badala ya kuyafungia moja kwa moja magazeti unaweza
kutengeneza utaratibu wa kuyakatia idadi ya nakala wanazoweza kuchapisha
na ukadhibiti kuwa wachapishe hizo tu, lengo hapa likiwa kuwaminya
kwenye mapato kwa siku kadhaa ili wajifunze. Adhabu ya kulizuia lisitoke
kabisa ama kulifungia milele zinakuwa ni za juu kabisa. Na kabla ya
kufikia uamuzi huo wanapaswa wawe wanajua kosa lao na adhabu zake, na
wasikilizwe na jopo maalum litakalosimamia utoaji wa adhabu hiyo, siyo
kuachia mamlaka yote kwa mtu mmoja tu, Waziri wa Habari, kama ilivyo
sasa.
Dkt. Hamisi Kigwangalla, MB ni Mbunge wa Jimbo la Nzega na pia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI). Ni mhitimu wa Digrii ya Udaktari wa Tiba za
Binadamu, Shahada za uzamili kwenye Afya ya Jamii (MPH) na kwenye
Usimamizi wa Biashara (MBA). Kwa sasa anaandika tasnifu yake ya digrii
ya Uzamivu(PH.D.) kwenye Afya ya jamii (mifumo ya usawa na uchumi wa
afya).