Sunday, August 4, 2013

UCHOCHEZI WA KUTISHA WA SHEIKH PONDA WAFIKIA PABAYA

 
SERIKALI imenasa kanda za video zinazomuonyesha Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, akitoa mahubiri yanayowahamasisha waumini wa dini ya Kiislamu kuanzisha uasi dhidi ya serikali.

Tukio la kunaswa kwa kanda hizo limekuja ikiwa ni siku chache baada ya Jeshi la Polisi Zanzibar kutangaza kumsaka Sheikh Ponda kwa tuhuma za uchochezi, akingali anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya Dar es Salaam kumkuta na hatia ya kosa la uchochezi.

Katika kanda hizo ambazo MTANZANIA Jumapili imefanikiwa kuziona, Sheikh Ponda, amerekodiwa akiwa katika Msikiti wa Mbuyuni, Zanzibar, alikohudhuria Mhadhara wa Dini ya Kiislamu, akiwataka waumini wa dini hiyo kuchukua hatua za kuikomboa Zanzibar kipindi hiki cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kutoka kwenye mikono ya utawala wa makafiri.


Huku akiitikiwa kwa neno Takbir kutoka washiriki wa mhadhara huo, Sheikh Ponda anasikika akisema Zanzibar ni nchi ya Kiislamu, hivyo Waislamu wana wajibu kwa kuikomboa kutoka mikononi mwa vibaraka wanaoiongoza, aliodai kuwa wananyonya uchumi wake na kuutoroshea nje ya visiwa hivyo.

Moja ya kanda hizo iliyorekodiwa kwa muda wa saa moja na dakika ishirini na nne, ambayo Sheikh Ponda alitumia muda mwingi kusisitiza umuhimu wa Waislamu kuikomboa Zanzibar kutoka mikononi mwa aliowaita makafiri, anasikika akisema:

“Mna wajibu wa kuikomboa Zanzibar na si mnaweka vibaraka, wanateuliwa huko halafu wanakuja hapa kuwaongozeni, fedha zote zinachukuliwa hapa na kupelekwa kule kwa sababu tumepoteza nchi, tumepoteza hadhi.

“Makafiri wanatakiwa kuyaheshimu mambo matakatifu ya Kiislamu na kuyajua, kama hawataheshimu Mwenyezi Mungu alisema lazima mlipize kisasi katika mambo matakatifu.
Mungu alisema ni lazima mlipize kisasi mwezi mtakatifu kwa mwezi mtakatifu. Mambo matakatifu yamewekewa kisasi.

“Miongoni mwa mambo matakatifu yaliyowekewa kisasi ni haki na uadilifu pamoja na dini ya Kiislamu, unapozungumzia dini ni pamoja na masheikh, hawa ni watu watakatifu, watu wenye hadhi, ni watu wakubwa na watakatifu kuliko baba mtakatifu kama wanavyosema wao.”

Sheikh Ponda pia anasikika akieleza kuwa Waislamu wamedhalilishwa kwa muda mrefu, hivyo wana wajibu wa kuikomboa Zanzibar kwa kuwa hata Mtume Mohammad aliongoza jeshi akakomboa nchi ya Maka kipindi cha Mwezi Ramadhani.

Alieleza kushangazwa na uteuzi wa Rais wa Zanzibar kufanyikia Dodoma na hata uamuzi wa kumuondoa madarakani kuchukulia mkoani humo na kutoa mwito wa jambo hilo kusitishwa.

Katika hili anasikika akisisitiza kuwa; “Hakuna mtu ambaye haelewi kwamba Zanzibar ipo mikononi mwa watu wasio stahiki, Zanzibar ni nchi ya Waislamu. Sisi Waislamu wa Zanzibar tuna mazingatio makubwa kuliko watu wengine kipindi hiki cha Mwezi Ramadhani kwa sababu mafundisho tunayoyapata katika maisha ya Mtume Mohammad ni sawa na mazingira ya sasa, hivyo tunatakiwa kuyatekeleza. Zanzibar si nchi ya watu, bali ni ya Waislamu.

Katika mahuburi yake kwenye mhadhara huo, Sheikh Ponda anakisika akieleza kuwa Muungano wa Zanzibar na Tanganyika umezaa ufisadi visiwani humo na kurejea kauli aliyodai kutolewa na Mtume iliyokuwa ikiwaonya Wazanzibari kutoruhusu uwepo wa Muungano.

“Tangu lini bia, ukahaba ukawa hitajio la Wazanzibari na hii ndiyo ‘product’ iliyotokana na Muungano na Mapinduzi.
Maovu ambayo hamkuyapata kuyaona ni kauli ya Mtume, alisema mkiruhusu muungano ufisadi unatokea. Leo hii mnaona nchi ya Zanzibar mambo ambayo si hitajio la Wazanzibari, mmeingiza watawala waovu katika ardhi hii.

“Zanzibar ina watu wenye akili kubwa, wenye uwezo na ina wasomi wa fani zote na ni watu wa kuigwa duniani kote…. hivi sasa Mwislamu anapokwenda mahakamani anayesikiliza shauri ni kafiri. Mwislamu anapofunguliwa kesi, sheria hazifuatwi kwa maana kwamba kuna utaratibu wa dhamana, lakini hautolewi, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwakandamiza Waislamu.

“Leo hii viongozi wetu wanatiwa jela bila sababu, kosa lao ni pale wanapotetea Uislamu
. Wako gerezani, tutapataje sifa ya Ramadhani tusipowatoa hawa ndugu zetu walioko gerezani na Mungu anasema mambo matakatifu yanalipiziwa kisasi.

“Kila siku viongozi wa Kiislamu wanauawa, Sheikh Hamis ameuawa anatoka msikitini,
kafa na hakuna maelezo kwa sababu kwa mujibu wa sheria, lazima kuwe na maelekezo na mahakama iseme. Yote hayo hakuna maelezo yoyote utadhani kafa paka, kapigwa risasi kafa hakuna maelezo yoyote ya serikali.

“Ndugu zangu hali ni mbaya sana, watu wanapanga mikakati kwa ajili yenu ninyi. Msifikirie kuwa jamii haiwezi kutoweka. 


'Tujenga utayari kwa ajili ya kupigania dini ya Mwenyezi Mungu, hilo ni jambo la msingi. Ukimya wenu ni tatizo kubwa sana, hivi ndivyo wanavyotaka wafike mahala wakamate mashekh wawaweke ndani, halafu mkae kimya, hili jambo ni kubwa na ni la dini, mnatakiwa msimame kidete kwa ajili ya jambo hili.

“Suala la kisasi lina uhusiano na uhai, mtapata uhai mzuri katika kulipiza kisasi ninyi Waislamu.”

Akizungumzia kukamatwa kwake hapo awali, alisema ulikuwa ni mkakati uliopangwa Dodoma, baada ya kusikilizwa kwa malalamiko ya waumini wa dini ya Kikristo.

Mbali na hayo, kauli nyingine zinazoelezwa na baadhi ya watu walioona na kusikiliza kanda hizo kuwa zina kila dalili ya kuhatarisha amani nchini, ni ile anayosikika akisema; “Sisi viongozi ndio tunatoa maagizo tuingie barabarani hata kama serikali imepiga marufuku. Kama wataleta jeshi sisi tunakuwa ‘front.’

“Kama wewe unaogopa polisi itakapofika Jihad utatoka, hawa ni watu kama wewe, anavyokupiga kirungu hakuna sababu ya kumwogopa binadamu mwenzako, hizo ni hatua za kujenga nafsi na utayari.

“Kipindi cha uchaguzi mkitumie vizuri, muwatoe hawa madarakani, watoeni wakatae halafu kimbembe kianze pale, mnatoa kauli ya moja kwa moja. Waambieni kuwa ninyi na sisi ni moto na baruti.

“Kwa upande wa Katiba, kuna suala la kupiga kura, hakikisheni kura yenu izingatie maslahi yenu. Kule Bara tulipendekeza mahakama ya kadhi imetupwa na sasa hivi kazi zile ambazo zinatakiwa kufanywa na mahakama ya kadhi zinafanywa na mahakama ya mwanzo.