Akizungumza na mwandishi wetu Jumatano ya wiki hii maeneo ya Mlimani City jijini Dar, msanii huyo alisema amesikitishwa na maamuzi ya bodi hiyo huku akidai kuwa lengo la filamu hiyo ni kukemea tabia za kishoga zinazoendelea kuibuka kwa vijana ikiwa ni pamoja na kupinga uhalali wa ndoa za jinsia moja.
Katika maelezo hayo, DK. Cheni ambaye huzitendea haki filamu zake kwa kuvaa uhusika halisi, alisema moja ya kigezo ambacho bodi hiyo imekitumia kuzuia filamu hiyo ni pamoja na muonekano wa bango la filamu hiyo ambalo linamuonesha msanii huyo akiwa amevaa vazi la shera huku akiwa amejiremba kwa madai kuwa ni kuchochea ushoga jambo ambalo msanii huyo amelipinga vibaya.
“Eti ushoga wangu uko kwenye kujiremba sana, hakika wamenionea sana, lengo letu ni kuonya na kukemea vikali vitendo vya ushoga na ndoa za jinsia moja, huwezi kuelimisha bila kuonesha madhara yake kwa vitendo kama ilivyo ndani ya filamu hiyo.
“Lakini, ndani ya filamu hiyo, kuna kipande ambacho kinaonesha kiongozi wa serikali akikemea kitendo hicho, sasa hapo ushoga wangu uko wapi? Kuvalia shera kwenye kava? Siyo sahihi,” alisema Dk. Cheni.
Mbali na kava hilo, msanii huyo alidai haoni kosa lolote katika filamu hiyo hivyo ataendelea kupigania haki yake na kwamba hayuko tayari kuonewa.