- Habari za uhakika ambazo Mwananchi imezipata kutoka ndani ya shirikisho hilo zimesema kuwa mfanyakazi huyo ametakiwa kutoa maelezo ya kutosha hadi ifikapo leo huku akitakiwa kutaja wahusika alioshirikiana nao kuhujumu mapato ya mchezo huo.
Mfanyakazi huyo ametakiwa kutoa maelezo ya kutosha hadi ifikapo leo.
Dar es Salaam.
Mfanyakazi mmoja wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) amekamatwa na
tiketi feki za mchezo wa Azam na Mbeya City uliofanyika wiki iliyopita
na timu hizo kutoka sare ya mabao 3-3 mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa
Azam Complex.
Habari za uhakika ambazo Mwananchi
imezipata kutoka ndani ya shirikisho hilo zimesema kuwa mfanyakazi huyo
ametakiwa kutoa maelezo ya kutosha hadi ifikapo leo huku akitakiwa
kutaja wahusika alioshirikiana nao kuhujumu mapato ya mchezo huo.
Chanzo
kimedai kuwa mfanyakazi huyo amekuwa akishirikiana na vigogo wengine wa
soka mtandao ambao umeota mizizi tangu uongozi uliopita wa TFF.
Sakata
la mfanyakazi huyo liliibuka kwenye kikao cha Rais mpya wa TFF, Jamal
Malinzi alipofanya mazungumzo na wafanyakazi wa shirikisho hilo
akiwahakikishia kuboresha maslahi yao na kuwataka kufanya kazi kwa uhuru
na amani na kuepuka kusikiliza maneno yanayoendelea hivi sasa huku
baadhi yao wakiwa hawajui hatma ya ajira zao.
Hata hivyo Mwananchi
ilipomtafuta Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Silas Mwakibinga kuhusiana na
suala hilo alisema “kuna mjumbe mmoja wa Kamati ya Utendaj alishtukia
mchezo mchafu ambao mfanyakazi wa TFF anaucheza getini wakati wa mechi
hiyo akamfukuza kukaa getini.
“Mbali na mfanyakazi huyo pia kuna
watu wawili ambao walikamatwa na walilala kituo cha Polisi Mbagala baada
ya kukutwa na vitabu viwili vya bei ya Sh 3,000. “Walichokuwa
wanakifanya hawa mabwana ni kwamba tiketi moja inachanwa mara mbili na
kuuziwa watu wawili tofauti kwa gharama ya sh 3000 kila moja.
Mwakibinga alidai watu hao wawili walikamatwa na walilala Polisi na kufunguliwa jalada lenye RB No. MBL/RB/11851/2013.
“Walighushi
tiketi kitabu namba 07901 hadi 08000 kikiwa na tiketi mia na sikumbuki
kitabu chake kilikuwa namba ngapi ili namba zake zilifuatana na hizo,”
alisema.