
Tume ya
Mabadiliko ya Katiba imeomba kuongezewa muda wa mwezi mmoja kutokana na
ugumu wa kazi ya uchambuzi wa maoni yaliyotolewa na wananchi na asasi
mbalimbali.
Tume hiyo
inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba ilitakiwa kufanya kazi kwa miezi 18
kwa mujibu wa Sura ya 83 ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Maana yake ni kuwa Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 1, mwaka jana ilitakiwa kukamilisha kazi yake Novemba 1, mwaka huu.
Ikiwa maombi hayo ya Tume yatakubaliwa ina maana watatakiwa kukabidhi ripoti yake Desemba 1, mwaka huu.
Makamu
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Augustine Ramadhan aliliambia gazeti hili
kwa simu jana kuwa wamepeleka serikalini maombi ya kuongezewa muda wa
kufanya kazi.
Hata hivyo, Jaji Ramadhan alisema kuwa wameomba muda zaidi kutokana na kukabiliwa na kazi kubwa ya kuchambua maoni hayo.
Alisema hakuwa na taarifa ya majibu ya kama ombi lao limekubaliwa au la.
"Hatukuomba
miezi miwili kama sheria inavyotuelekeza, tumeomba mwezi mmoja na mpaka
Ijumaa nilipotoka ofisini sikuwa na taarifa kama kibali kilikuwa
kimetolewa, labda kesho (leo) nikienda ofisini nitafuatilia kufahamu
kama kimetoka," alisema Jaji Ramadhan.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alikiri kuwa tume hiyo imeomba kuongezewa muda.
"Ni kweli barua ya Tume imeletwa, tumeipokea na inafanyiwa kazi," alisema Rweyemamu kwa kifupi.
Waziri wa
Sheria na Katiba, Mathias Chikawe akizungumza kwa njia ya simu; baada ya
kuulizwa ikiwa Serikali imetoa kibali hicho au la alisema, "Sizungumzi
na waandishi leo." Simu ikakatika.
Ahadi ya Warioba yashindwa kutekelezeka
Hatua hiyo
inatofautiana na ahadi ya Jaji Warioba, ambaye mara nyingi amekuwa
akisisitiza kuwa tume yake itamaliza kazi yake katika muda uliopangwa.
Jaji Warioba alitoa ahadi hiyo kwa mara ya mwisho wakati akizungumza na vyombo vya habari Septemba 26, mwaka huu.
"Mipango ya
tume ni kukamilisha kazi hii ndani ya muda uliowekwa na Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba katika Sura ya 83," alieleza Jaji Warioba wakati
huo.
Tume imefuata sheria
Tume imeomba kuongezewa muda kama inavyoelekezwa kwenye kifungu cha kidogo cha (4) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
"Endapo Tume
itashindwa kukamilisha kazi yake ndani ya kipindi kilichoelezwa katika
kifungu kidogo cha (3), Rais kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar,
anaweza kuongeza muda usiozidi miezi miwili ili kuiwezesha Tume
kukamilisha na kuwasilisha ripoti," kinaeleza kifungu kidogo hicho.
Bunge la Katiba na Kura ya Maoni sasa kuchelewa
Kutokana na ombi hilo la tume, maana yake sasa mkutano wa Bunge la Katiba utasogezwa mbele.
Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ilitakiwa kukabidhi kazi yake Novemba 1, lakini kwa
kuomba muda ina maana wataathiri ratiba ya mkutano wa Bunge la Katiba.
Bunge la Katiba lilitakiwa kukutana katikati ya mwezi Novemba kujadili Rasimu ya pili ya Katiba baada ya kuwasilishwa na tume.
Maana yake sasa Bunge la Katiba kuna uwezekano mkubwa likakutana mwakani au Desemba mwishoni.
Pia suala hilo litaathiri mpangilio wa kura ya maoni, ambayo inatakiwa kuitishwa baada ya Bunge la Katiba kupitisha rasimu.
Ombi hilo kwa
kiasi kikubwa linaweza kuathiri mchakato wa kupata Katiba ya Tanzania
Bara ikiwa Katiba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Serikali tatu
itapitishwa na wananchi.
Chanzo:Mwananchi