
"Jamani pesa
yenu iliyoibiwa hii hapa," Ni kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Iringa
ACP Athmani Mungi akiwaonyesha raia wa China maburungutu ya fedha
zilizonusurika kutoka kwa majambazi waliowateka na kuwapora raia wa
China.

Fedha shilingi
Milioni 80 ambazo zimerejeshwa na jeshi la polisi kutoka mikononi wa
majambazi wa tukio la utekaji wa raia wa Kichina, waliovamiwa katika
mlima wa Nyang'olo mkoani Iringa.

Kamanda Mungi
akiwa ameshika Silaha aina ya ShortgunGreener ambayo imekatwa Mtutu
(kitako) silaha iliyotupwa na watu wanaosadikika kuwa ni majambazi baada
ya kuzidiwa nguvu na askari polisi katika mapambano ya kuokoa fedha za
raia wa China.

Mamilioni ya
fedha yakiwa yameshikwa na kamanda wa jeshi la Polisi mkoni Iringa, mara
baada ya kusalimika kutoka mikononi mwa majambazi, ambao walipora
vitita vya fedha hizo kutoka kwa raia wa China.

Raia wa China
wakiwa na askari polisi katika ukumbi wa ofisi ya kamanda wa jeshi la
polisi wakipewa taarifa za kupatikana kwa baadhi ya fedha zao na vifaa
walivyoporwa na watu wanaosadikika kuwa ni majambazi.(P.T)

Raia wa China
wakiwa katika ofisi ya kamanda wa jeshi la Polisi mko wa Iringa,
wakifurahia kuziona fedha zao ambazo zilikuwa zimepolwa na majambazi
katika mlima wa Nyang'olo Wilaya ya Iringa, wengine ni askari wa jeshi
la Polisi.
WATU
wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wamewateka raia wanne wa China mkoani
Iringa, na kisha kuwapora fedha, zaidi ya shilingi Milioni 130 za
Kitanzania, fedha za Kichina, pamoja na vifaa mbalimbali zikiwemo simu
tano katika mlima wa Nyang'oro uliopo mkoani Iringa.
Akizungumzia
tukio hilo kamanda wa jeshi la Polisi mkoani Iringa ACP Athmani Mungi
amesema raia hao wa china wa kampuni ya SIETCO, inayojenga barabara ya
Iringa- Dodoma, walikutwa na mkasa huo wakati wakirejea kutoka Iringa
mjini, ambapo msako mkali wa jeshi hilo umefanikisha kupatikana kwa
shilingi Milioni 80.
ACP Mungi
amesema wachina hao walitekwa na kuporwa kiasi hicho cha fedha na vitu
mbalimbali, mara baada ya kuchukua fedha hizo katika benki ya CRDB tawi
la Iringa, na wakiwa katika gari lao aina ya Toyota yenye namba za
usajili T. 335 CMX lilizuiliwa na gari kubwa aina ya Lori katika mlima
wa Nyang'olo huku watu watano wenye siraha wakapora mfuko uliokuwa na
fedha hizo.
Amesema
majambazi hao walichukua pia simu za mkononi tano na funguo za gari la
wachina na kutokomea nalo pamoja na kiasi hicho cha fedha cha shilingi
Milioni 135, ambazo walikuwa wanarudi
nazo katika kambi yao ya Mtera.
"Wachina hao
walikuwa wametoka kuchukua fedha hizo katika benki ya CRDB tawi la
Iringa mjini bila kuwa na ulinzi wowote wa askari Polisi, na walikuwa
wanazipeleka katika kambi yao iliyopo
Mtera," Alisema Mungi.
Amesema jeshi
la polisi baada ya kupata taarifa hiyo walifanya oparesheni la kuwasaka
majambazi hao mchana na usiku, kwa kushirikiana na wananchi wa vijiji
vya tarafa ya Isimani, ambapo zoezi hilo liliendelea mpaka siku ya
tarehe 23 alfajiri walipowaona majambazi hao.
"Oparesheni ya
kuwasaka majambazi waliofanya tukio hilo iliendelea usiku na mchana,
askari polisi kwa kushirikiana na wananchi, na alfajiri ya leo majira ya
saa kumi askari yaliyaona majambazi hayo na ndipo mapambano makali
yalianza, huku majambazi na askari wakirushiana risasi za moto,"
Alisema.
Pia amesema
mapambano makali yaliwachanganya majambazi hayo na kupelekea kutupa
Silaha aina ya Shortgun Greener iliyokuwa imekatwa Mtutu (Kitako) ikiwa
na risasi moja chemba, huku majambazi hayo yakitupa begi moja
lililokutwa na shilingi Milioni 80, na lingine likiwa na Biscuit na vitu
vingine vya kichina.
Mungi amesema
katika oparesheni hiyo pia wamefanikiwa kumkatata jambazi mmoja ambaye
hakutaka jina lake litajwe kwa kuhofia kuharibu upelelezi wa kuwasaka
majambazi wengine wanne waliofanikiwa kutoroka.
Mungi amesema
jambazi huyo amekamatwa katika kijiji cha Itono akiwa katika gari aina
ya Hiace na kukutwa na Pochi ya wachina ambayo ilikuwa na vitu
vilivyoibwa kwenye eneo la tukio hilo la
utekaji.
"Vitu
alivyokutwa navyo mtu tuliyemkamata ni fedha za kichina zinazofahamika
kama Yuan zikiwa 97, nyingine ni fedha hizo hizo za kichina zinaitwa
Jiao hizo zilikuwa tatu, leseni ya udereva mali ya mchina Gang Cheng,
Leseni ya udereva ya Hua -Li-wei, Simu moja ya kichina pamoja na
Vitambulisho vilivyoandikwa kwa lugha ya Kichina," Alisema Mungi.
Aidha kamanda
Mungi ametoa onyo kwa majambazi kuacha mara moja uharifu kwa madai kuwa
mkoa wa Iringa si salama kwa majambazi na waharifu wa aina yoyote kwani
hata wanaotoka nje ya mkoa huo wakiingia kufanya uharifu hawatatoka
salama, huku akiwaasa wananchi kuacha mara moja kusafiri na fedha kiasi
kikubwa pasipokuwa na ulinzi wowote.
Pia Kamanda
Mungi amewashukuru wananchi walioshirikiana na jeshi la polisi katika
kufanikisha zoezi la kupatikana kwa fedha hizo, pamoja na baadhi ya vitu
vya wachina hao.
Hata hivyo
siku za hivi karibuni, gari la kampuni ya E. Awadhi, kampuni
inayojihusisha na usafirishaji wa mafuta nchini Zambia na Malawi
lilitekwa katika eneo la Igumbilo mjini Iringa na kisha
watekaji
kutoroka na gari ambalo lilikuwa limejaza mafuta katika mataki yake,
huku jeshi hilo likifanikiwa kumnasa mmoja wa watuhumiwa wa tukio hilo.
MWISHO
Chanzo:Oliver Motto