
Jumla ya dawa
bandia za aina 273 zenye thamani ya shilingi 49,634,733/= zimekamatwa
katika operesheni maalumu iliyoendeshwa na Jeshi la Polisi kwa
kushirikiana na Shirikisho la Polisi la Kimataifa (Interpol), Baraza la
Famasi, TAMISEMI, Bohari ya Dawa (MSD), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF), Shirika la Viwango (TBS), Tume ya Ushindani (FCC), Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP),
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Rais na
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika maeneo 138 nchini.
Operesheni hiyo ijulikanayo kama 'Giboia' iliendeshwa kwa lengo la kufuatilia, kukamata na kuwafikisha katika vyombo vya
sheria wanaojihusisha na biashara ya dawa bandia, zisizosajiliwa, zisizo na ubora na zilizoisha muda wa matumizi.
Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba alisema hayo
alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana wakati
akitangaza matokeo ya operesheni hiyo. Alisema operesheni hiyo
ilifanyika kwa siku tatu, Oktoba 1-3 mwaka huu, kwa kukagua maduka ya
dawa ya jumla na rejareja, waingizaji wa dawa nchini, vituo vya afya na
maabara binafsi.
Aliyataja
maeneo , ambayo ukaguzi huo ulifanyika na idadi ya vituo kwenye mabano
kuwa ni Dar es Salaam (67), Mbeya (6), Kilimanjaro (8), Arusha (5),
Mwanza (11), Geita (7), Shinyanga (6) na Dodoma (20).
"Dawa bandia
zilizokamatwa zilikuwa aina mbili (Asdoxin na Penizin-V), zilizoisha
muda wa matumizi zilikuwa 76, dawa za serikali na miradi mbalimbali ya
serikali 28, zisizosajiliwa 86 na zenye ubora duni 40," alisema.
Alisema dawa
nyingine ni zilizofutiwa usajili 41 na 19 zinazohisiwa kuwa ni bandia,
ambazo zilikamatwa na kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara kuhakiki ubora
wake.
Manumba alisema hatua zimechukuliwa, ikiwa ni pamoja na majalada 42 ya kesi kufunguliwa katika vituo mbalimbali nchini.
Manumba alisema hatua zimechukuliwa, ikiwa ni pamoja na majalada 42 ya kesi kufunguliwa katika vituo mbalimbali nchini.

MAELEZO YA
UTANGULIZI YA MKURUGENZI MKUU WA MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA (TFDA) BW.
HIITI B. SILLO KATIKA MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MATOKEO YA
OPERESHENI "GIBOIA" KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA TFDA TAREHE 10 OKTOBA,
2013
Naomba
nichukue fursa hii kwa niaba ya Menejimenti na Wafanyakazi wa TFDA
kuwakaribisha, katika ofisi za Mamlaka ya Chakula na Dawa. TFDA ni
taasisi iliyo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii yenye jukumu la
kudhibiti ubora na usalama wa vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba.
Naamini wote
tunaelewa dhima ya TFDA ambayo ni kulinda afya za wananchi kwa kuzuia
athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya vyakula, dawa,
vipodozi na vifaa tiba. Katika kufikia dhima hii, changamoto kubwa
tunayokabiliana nayo katika udhibiti ni uwepo wa bidhaa duni, bandia na
zisizosajiliwa kwenye soko.
Ndugu wanahabari,
Tumewaalika
ili tuwape taarifa juu ya matokeo ya Operesheni Giboia iliyofanyika hapa
nchini kwa pamoja baina ya Mamlaka ya Chakula na Dawa na Jeshi la
Polisi nchini kwa kushirikiana na Shirikisho la Polisi la Kimataifa
(Interpol) na taasisi na idara nyingine za Serikali. Taasisi na idara
nyingine za Serikali ambazo majukumu yake yanagusa masuala ya dawa au
udhibiti zilizoshiriki operesheni hii ni mpamoja Baraza la Famasi,
TAMISEMI, Bohari ya Dawa (MSD), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),
Shirika la Viwango (TBS), Tume ya Ushindani (FCC), Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP), Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Rais na Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii.
Napenda
kuzishukuru taasisi hizi kwa ushirikiano wao katika kufanikisha
operesheni mbalimbali za kupambana na biashara haramu ya dawa bandia na
kwa namna ya pekeeOperesheni Giboia. Mamlaka itaendelea kushirikiana na
taasisi hizi katika kukabiliana na changamoto ya udhibiti wa bidhaa
bandia na duni za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba bandia na vile
ambavyo havisajiliwa na Mamlaka ili kuwalinda wananchi dhidi ya madhara
ya kiafya wanayoweza kuyapata.
Ndugu wanahabari,
Operesheni hii
ni mwendelezo wa operesheni za awali za kufuatilia dawa bandia na duni
katika soko. Lengo la Operesheni hii lilikuwa ni kukamata na kuwafikisha
katika vyombo vya sheria wale wote wanaojihusisha na biashara ya dawa
bandia. Dawa zilizolengwa zilikuwa ni dawa za kutibu ugonjwa wa malaria,
dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi, viuavijasumu
(antibiotics), dawa za kuongeza nguvu za kiume na dawa za kupunguza
maumivu. Dawa hizi zilichaguliwa kutokana na kuwa na matumizi makubwa
zaidi hapa nchini na hivyo kuwa na soko kubwa kiasi cha kuvutia biashara
haramu ya dawa bandia. Vile vile, katika Operesheni hii dawa za
Serikali na miradi mbalimbali ya Serikali, dawa zisizosajiliwa, dawa
duni na dawa zilizoisha muda wa matumizi zilifuatiliwa.
Ndugu wanahabari,
Operesheni
Giboia imefanyika sanjari katika nchi saba zilizopo kusini mwa Jangwa la
Sahara ambazo ni Afrika Kusini, Angola, Malawi, Msumbiji, Swaziland,
Zambia na Tanzania kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 1 hadi 3 Oktoba
2013.
Makubaliano ya
kufanyika kwa Operesheni Giboia yalifikiwa katika mkutano uliohusisha
nchi nilizozitaja uolifanyika jijini Luanda, Angola tarehe 10 hadi 12
Juni 2013. Pamoja na mambo mengine, mkutano huo uliweka mikakati ya
namna ya kuendesha Operesheni Giboia kwa mafanikio.
Napenda
kuwajulisha kwamba ushirikiano baina ya nchi mbalimbali katika vita
dhidi ya dawa bandia ni utekelezaji wa Azimio la Mawaziri wa Afya
Duniani la mwaka 2012 (World Health Assembly Resolution 65.19). Azimio
hilo pamoja na mambo mengine limeelekeza ushirikiano wa kikanda na
kimataifa katika kupambana na biashara haramu ya dawa bandia.
Kwa upande wa
Tanzania, Operesheni Giboia imefanyika katika mikoa tisa ya Mwanza,
Shinyanga, Mara, Geita, Mbeya, Arusha, Kilimanjaro, Dodoma na Dar es
salaam. Maeneo yaliyokaguliwa ni pamoja na famasi, maghala ya kutunzia
dawa, vituo vya afya na maabara binafsi na maeneo yote yaliyotiliwa
mashaka ya kuwepo kwa dawa hizo bandia.
Ndugu wanahabari,
Kwa kumalizia
maelezo yangu, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, Kamishna wa Polisi, Bw. Robert
Manumba na Jeshi la Polisi kwa ujumla kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa
kwa TFDA katika kupambana na tatizo hili kubwa la dawa bandia katika
nchi yetu. Aidha, natoa shukrani za dhati kwa taasisi na vyombo vyote
vya dola kwa ushiriki wao katika operesheni hii na vile vile kwa kuwa
tayari wakati wote kushirikiana na TFDA katika mapambano haya. Imani
yangu ni kwamba ushirikiano uliopo ukiendelezwa na kwa ushirikiano
kutoka kwa wanahabari na wananchi kwa ujumla tutashinda vita dhidi ya
biashara haramu ya dawa bandia.
Baada ya
maelezo haya, ninayo heshima kumkaribisha Kamishna wa Polisi, Robert
Manumba, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini ili aweze kutoa matokeo ya
Operesheni Giboia.
Asanteni kwa kunisikiliza.