
Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda ametengua tangazo la Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi
Kagasheki la kuligawa eneo la Pori Tengefu la Loliondo, Wilaya
yaNgorongoro, mkoani Arusha kwa kutenga kilomita za mraba 1,500 kwa
ajili ya uhifadhi na kilomita za mraba 2,500 kuwa chini ya Serikali za
vijiji.
Machi
19, mwaka huu, Waziri Kagasheki alitoa tangazo la Serikali la kuligawa
pori hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 4,000 ili Serikali iweze
kuhifadhi eneo la kilomita za mraba 1,500 ambalo alieleza kuwa ni mapito
na mazalia ya wanyamapori, pia kutunza ikolojia ya Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti. Tangazo hilo liliibua mgogoro mkubwa.(P.T)
Akizungumza katika
mkutano wa hadhara katika eneo la Waso jana baada ya kutembelea eneo la
mgogoro na kufanya kikao na ujumbe wa mawaziri alioambatana nao na
watendaji wa wizara mbalimbali, Waziri Mkuu alisema amefikia uamuzi wa
kuondoa tangazo hilo la Serikali na sasa wananchi wa eneo hilo
wataendelea na utaratibu uliozoeleka.
Mawaziri waliokuwa
katika ziara hiyo ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera,
Uratibu na Bunge),William Lukuvi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilith Mahenge, Naibu Waziri
wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Benedict Ole Nangoro na Naibu Waziri
(Tamisemi), Kassim Majaliwa.
"Mara baada ya lile
tangazo kuliibuka mgogoro wa wananchi kupinga na baadhi ya viongozi
walinifuata hadi Dodoma na kuniletea malalamiko yao. Pia CCM iliunda
tume na kunipa taarifa lakini nikasema siwezi kutoa uamuzi hadi nifike
mwenyewe katika eneo hili na sasa nakubaliana na hoja za wananchi kuwa
kuligawa eneo kutakuwa na athari kwenu, naomba sasa mwendelee na
utaratibu wenu kama vile halikuwepo tangazo hilo," alisema Pinda.
Alisema miongoni mwa
hoja za wananchi zilizosababisha afikie uamuzi huo, ni kuwa eneo hilo la
kilomita za mraba 1,500 ndilo ambalo lina vyanzo vya maji
vinavyotegemewa na vijiji vyote sita ambavyo vingeathiriwa na tangazo
hilo. Vijiji hivyo ni Ololosokwani, Soitsambu, Olorieni Magaiduru,
Arash, Piyaya na Oloipili.
Waziri mkuu pia
alisema eneo hilo lililotengwa kwa uhifadhi ndilo tegemeo la wananchi
kwa ajili ya malisho ya mifugo hasa nyakati za kiangazi, pia kuna makazi
ya watu, shule na huduma nyingine muhimu.
Alisema kutokana na
uamuzi huo, Serikali inajipanga kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi
katika wilaya hiyo ili kutambulika maeneo ya ufugaji, makazi, kilimo na
uhifadhi ili masilahi ya kila upande yaendelee kulindwa.
"Utaratibu wenu
mliojiwekea kabla ya tangazo la Serikali uendelee kwani tunataka
shughuli za uwindaji wa kitalii ziendelee, upigaji picha uendelee, pia
ufugaji uendelee na hapa ni vyema kukawa na vikao vya wadau wote walau
kila baada ya miezi mitatu," alisema Pinda.
Waziri Mkuu aliagiza
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Halmashauri ya Ngorongoro kuratibu
vikao hivyo kwani lengo ni kutatua migogoro na kurejesha uhusiano.
Mara baada ya Waziri
Mkuu kutangaza uamuzi huo, shangwe zilitawala na Mbunge waNgorongoro,
Saning'o ole Telele na madiwani wakiongozwa na Mwenyekiti wa
Halmashauri, Elias Ngolisa walieleza kuridhishwa na uamuzi huo wakisema
umezingatia kilio cha mamia ya wananchi wa Tarafa za Loliondo na Sale.
Mkurugenzi wa Kampuni
ya Ortello Business Co operation (OBC), ambayo ingebaki katika eneo
lililokuwa limetengwa kwa uhifadhi, Isack Mollel alisema hapingi uamuzi
huo lakini anataka mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) wilayani
Ngorongoro, kukubali mwafaka huo pia kushiriki katika vikao vya kupanga
matumizi bora ya ardhi vijijini muda ukifika.
Hata hivyo, kabla ya
kutangazwa kwa uamuzi huo, Mollel alisema Serikali isipotenga sasa
maeneo ya uhifadhi na ufugaji, shughuli za utalii zitakufa Loliondo
sambamba na kuathirika eneo zima la ikolojia la Serengeti kwani mifugo
imeongezeka na imeanza kuingia hadi ndani ya Hifadhi ya Serengeti.
Profesa Tibaijuka atoa suluhu
Awali, Profesa
Tibaijuka alisema suluhu ya migogoro ya ardhi Loliondo ni kuwa na
mipango ya matumizi bora ya ardhi baada ya vijiji kupimwa kazi ambayo
alikwishaianza.
Alisema umefika wakati pia kwa wafugaji wa Loliondo kupunguza mifugo na kuanza kufuga kisasa kwani ardhi haiongezeki.
Chanzo:Mwananchi.