Serikali ya Tanzania, imeiomba Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu
(ICC) kuruhusu Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto kutohudhuria baadhi
ya mashauri ya kesi yake ili kuweza kutimiza majukumu mengine ya
kiserikali.

Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, Jaji Fredrick Mwita
aliandika barua kwenda ICC Jumatatu wiki hii akitetea hoja ya Ruto
kutaka asihudhurie baadhi ya vikao vya kesi hiyo.
Katika barua yake, Jaji Werema alisema kuruhusu
Ruto kutohudhuria baadhi ya vikao vya kesi kutaimarisha ushirikiano
baina ya ICC na washirika.
Hata hivyo, maombi hayo yanayotaka Ruto kuruhusiwa
kutohudhuria kesi hiyo binafsi yamesimamishwa baada ya mwendesha
mashtaka wa ICC, Fatou Bensouda kuyawekea pingamizi na sasa yanasubiri
uamuzi wa majaji.
Hii ni mara ya pili kwa Tanzania, kuwasiliana na
ICC kwani iliwahi kuwasilisha ombi la kutaka kesi hiyo ya kina Ruto
isikilizwe Tanzania au Kenya.
Hata hivyo, mpango huo ulikwama baada ya majaji kuupinga kwa kura za hapana.
Mwandishi Sang ajitetea
Mwandishi wa habari wa kituo cha KASS FM Joshua
Arap Sang, amekamilisha ungwe ya kwanza ya utetezi wake kwenye Mahakama
ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na kueleza kuwa hakuhusika kwa namna
yoyote kuchochea machafuko yaliyojiri baada ya uchaguzi nchini Kenya.
Sang aliwasilisha utetezi wake katika hali ya
kujiamini huku akionyesha sura yenye matumaini na kuiambia mahakama
kuwa, kesi inayomkabili imetengenezwa ili kukatiza ndoto yake ya kuwa
mtangazaji bora duniani .
Mwandishi huyo ambaye anatetewa na mawakili
wanaoongozwa na Wakili Katwa Kigen, alipangua hoja zilizowasilisha na
upande wa mashtaka kwa kutumia historia ya maisha yake aliyoyaelezea
kuwa ni ya kumcha Mungu na uadilifu.
Kama ilivyo kwa washtakiwa wengine, Rais Uhuru
Kenyatta na Naibu wake William Ruto, Sang anadaiwa kuratibu na kupanga
mashambulizi na kusababisha zaidi ya watu elfu moja kupoteza maisha.
Pia anadaiwa kuendesha kampeni ya uchochezi kupitia vipindi mbalimbali vya redio baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2007.