Waziri Mkuu
mstaafu, Fredrick Sumaye, amewashukia ‘vigogo’ wenye madaraka, kuwa
wanahusika kushamirisha biashara ya dawa za kulevya, wakiwatumia vijana
katika kufikia malengo yao.
Sumaye amesema,
mbali na ‘vigogo’ hao, biashara hiyo inawahusisha baadhi ya
wafanyabiashara wenye nguvu kubwa za kiuchumi, na kusisitiza hakuna
sababu kwa jamii kuogopa ama kulifumbia macho tatizo hilo.
Hata hivyo,
Sumaye ambaye ni kiongozi pekee aliyehudumu wadhifa wa Uwaziri Mkuu kwa
muda mrefu (miaka 10), hakuwataja kwa majina vigogo ama wafanyabiashara
hao.
Lakini katika
siku za hivi karibuni, kumekuwapo taarifa zinazowahusisha baadhi ya
wanasiasa, akiwamo Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM) ambaye hata
hivyo, alikana kuhusika katika biashara hiyo.
Pia, aliyewahi
kuwa Mbunge kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM),
marehemu Amina Chifupa, aliwahi kutamka kuhusu kuwapo viongozi,
wanasiasa na wafanyabiashara wanaojishughulisha na biashara hiyo,
akitaka serikali iwashughulikie.
“Hili ni tatizo
ambalo hatuwezi kulifumbia macho. Biashara ya dawa za kulevya inafanywa
na watu wazito ama kwa fedha zao au kwa madaraka yao,” alisema Sumaye.
Sumaye alikuwa akizungumza katika uzinduzi wa Kituo cha Maendeleo ya vijana (Tayodec) mjini Arusha jana.
Alisema hivi sasa nchi inaonekana kuwa kituo muhimu cha kupitishia dawa hizo kwenda ama kutoka katika mataifa mengine.
“Hii siyo sifa
nzuri kwa nchi yetu. Lakini ukiachilia mbali madhara ya kupitishia
nchini, dawa hizo zinawathiri sana vijana wetu na kuwageuza mazezeta kwa
baadhi ya wale wanaozitumia,” alisema.
Kwa mujibu wa
Sumaye, uhalifu mwingi wa kutisha unafanywa na watu wanaozitumia dawa
hizo, huku vijana wanatumika kuzibeba kwenye miili yao, hali
inayohatarisha maisha yao ikiwamo kufa.
“Cha kusikitisha
wenye biashara hiyo wao hawaendi kuleta hizo dawa wala hawawatumii
watoto wao, bali watoto wa wenzao ili wakikamatwa na vyombo vya dola au
kudhurika kwa ubebaji huo, iwe ni shauri yao,” alisema.
“Hii ni roho
mbaya tena ya kinyama sana, kuona wewe kupata fedha hizo chafu kwa
gharama ya mtoto wa mtu mwingine, ati ni sawa tu. Lazima tujali watoto
wa wenzetu kama watoto wetu,” aliongeza.
ASEMA ANAHUJUMIWA KWA VIJANA
Sumaye alisema
Tayodec ni taasisi inayoshughulika na vijana, ikimteua kuwa mlezi wake,
lakini akipata upinzani kutoka kwa watu wasiomtakia mema.
Alisema watu hao (hakuwataja majina), wameiona taasisi hiyo kama mtaji wa kisiasa na kutaka kuitumia kwa malengo hayo.
“Najua
mmeshawishiwa kwa ahadi ya fedha nyingi na wakati huo huo kunikejeli
mimi kuwa sina fedha. Nadhani hawakujua kuwa moja ya malengo makuu ya
taasisi ni kupiga vita rushwa na tabia ya kununua watu na mngekubali
kununuliwa basi ndiyo ungekuwa mwisho wa taasisi yenu,” alisema.
WAWILI WASIMAMISHWA JNIA
Wakati Sumaye
akitoa angalizo hilo, maofisa wawili wa kitengo cha ukaguzi katika
Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam,
wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi unaohusishwa na kukamatwa kwa dawa
za kulevya nchini Afrika Kusini.
Hivi karibuni,
wasichana wawili wa Tanzania, Agnes Jerald (25) maarufu kama Masogange
na Melisa Edward (24), walikamatwa nchini humo wakiwa na dawa za kulevya
aina ya Crystal Methamphetamine, zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8,
zikitokea hapa nchini.
Washitakiwa hao
ambao walikatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo
uliopo jijini Johannesburg, wakiwa na kilo 150 za dawa hizo
zilizohifadhiwa kwenye masanduku sita.
Kaimu Mkurugenzi
wa JNIA, Poul Rwegasha, aliimbia NIPASHE Jumapili kuwa kufuatia sakata
la dawa hizo, wamewasimamisha kazi maofisa hao ambao hakuwataja majina
wala taasisi wanazofanyia kazi, ili kupisha uchunguzi.
“Siku ya tukio
hilo, tuliangalia kamera za usalama (CCTV) na kuwaona maofisa hao, hivyo
tumewasimamisha kwa ajili ya uchunguzi na siyo kwamba wamefukuzwa
kazi,” alisema.
Alisema kwa
hatua hiyo, wameondolewa kwenye kitengo cha ukaguzi, ingawa bado
wanafika kazini wakati uchunguzi dhidi yao ukiendelea.
Kwa mujibu wa Rwegasha, maofisa wawili wa polisi, ni miongoni mwa walioonekana kwenye CCTV hiyo, ingawa hakutaja majina yao.
Alisema hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kuhusu kuhusika kwa askari hao, hivyo uchunguzi ukikamilika hatua zinazostahili zitachukuliwa.
“Siyo vizuri
kukutajia majina ya hao maofisa kwani utaharibu uchunguzi wetu, na bado
hawajakutwa na hatia, uchunguzi utakapokamilika nitakupatia taarifa,”
alisema.
Kamanda wa
Polisi Viwanja vya Ndege, Deusdedit Kato, alisema zaidi ya watu 10
wamehojiwa kuhusiana na tukio hilo, na kwamba watajulikana pindi
uchunguzi utakapokamili.