Mfalme
Mswati wa Swaziland akisindikizwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati
alipoondoka kwenye uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini
Dar es salaam kurejea nyumbani baada ya kufungua maonyesho ya Biashara
ya Kimataifa kwenye uwanja wa Mwalimu Nyerere Julai 1,2013.
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akiagana na mfalme Mswati wa Swaziland ambaye
aliondoka nchini baada ya kufungua maonyesho ya Kiataifa ya Biashara
kwenye uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam Julai 1,
2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
---------
MFALME Mswati (III) wa Swaziland amewataka Watanzania kubadilika kwenda
sambamba na Soko la Pamoja la Afrika Mashariki kwa kubuni bidhaa
mbalimbali zenye ubora.
Alisema watanzania pia wanapaswa kuzipa
kipaumbele bidhaa zinazozalishwa nchini kwa lengo la kushindana katika
biashara duniani.
Mswati aliyasema hayo jana wakati akifungua Maonyesho ya 37 ya
Kimataifa ya Biashara katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, barabara ya
Kilwa, Dar es Salaam .
Alisema endapo wafanyabiashara wataibua
bidhaa zenye ubora na kuziendeleza itasaidia nchi kukua katika uchumi
pamoja na kunufaika na Soko la Pamoja la Afrika Mashariki (EAC).
Tanzania
ni miongoni mwa nchi tajiri na endapo kama itazingatia bidhaa
zinazozalishwa na wananchi wake uchumi wa nchi utakuwa kwa kasi na nchi
itahesabika kama ni miongoni mwa nchi tajiri duniani.
“Maonyesho
haya yanatoa fursa kwa watanzania kubuni na kujifunza mbinu mbalimbali
za biashara kufanya ushindani wa biashara duniani,”alisema Mswati.
Pia
alisema maonyesho hayo yanatoa fursa ya kuendeleza bidhaa zenye ubora
wa hali ya juu ikiwa ni miongoni mwa agenda kuu ya mdahalo waliojadili
viongozi mbalimbali wa ushirikiano wa biashara.
Alisema anaamini
serikali ya Tanzania inatoa kipaumbele kwa bidhaa zinazozalishwa nchini
zinazoingizwa katika soko la ndani kwa sababu kufanya hivyo kutasaidia
kuinua uchumi wa nchi.
Mfalme Mswati alisema anaamini ushirikiano
kati ya Tanzania na Swaziland utadumu ikiwa ni pamoja na kutangaza
bidhaa za ndani na kuutangaza utamaduni wa nchi.