Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amemtuhumu Mbunge
wa Monduli Edward Lowassa kwamba anahusika na kipigo alichokipata
kutokana na chuki aliyonayo kwake.
Aidha amemtuhumu Spika wa Bunge, Anne Makinda kwamba naye ni miongoni
mwa watu wanaomchukia pamoja na viongozi wengine wa Bunge, kwa kuwa
hakuna kati yao aliyempigia simu au kumtumia ujumbe wa kumjulia hali
kutokana na kipigo alichopata ambacho kimemsababishia maumivu makali.
Akizungumza
jana akiwa kwenye chumba alicholazwa katika Taasisi ya Tiba ya Magonjwa
ya Mifupa na Ufahamu Muhimbili (Moi), Nassari alidai Lowassa ambaye
amewahi kuwa waziri mkuu kabla ya kujiuzulu, amemchukia tangu
alipomshinda mkwewe Sioi Sumari, kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge
uliofanyika Aprili mwaka jana.
Nassari aliyekuwa amelazwa
katika Hospitali ya Selian ya jijini Arusha kabla ya kuhamishiwa MOI,
alidai kupigwa na kuchaniwa nguo na Green Guard wakati alipokuwa katika
jitihada zake za kuhesabu kura kwenye uchaguzi wa udiwani wa Kata ya
Makuyuni-Monduli.
“Kipigo nilichopata Lowassa anahusika
ananichukia, anataka urais lakini hawezi kuupata kwa kuuumiza watu kama
hivi, alifikiri kwamba nitakufa sitakufa hadi kwa mapenzi ya Mungu,”
alisema.
Alisema kuna jambo ambalo wananchi wanapaswa kulifikiria
ni jinsi ambavyo kumekuwa na matukio ya kutekwa na kuvamiwa, lakini
hakuna yanayohusisha kiongozi wa CCM, badala yake ni raia wa kawaida na
viongozi wa dini na siasa. Nassari alidai akiwa kama wakala mkuu wa
Chadema katika kata hiyo, alikumbana na mambo kadhaa yaliyomshangaza,
ikiwa ni pamoja na kufanyiwa jaribio la kutekwa mara mbili, kabla ya
kushambuliwa kwa kipigo.
Alisema pia anashukuru kwamba askari
wawili waliokuwepo katika eneo hilo walijitahidi kutaka kumnusuru,
lakini walizidiwa nguvu na vijana hao, hasa kutokana na kutokuwa na
bunduki, ambapo yeye alipofanikiwa kuchoropoka alikimbilia bastola yake
na kuwanyoshea vijana hao bila kufyatua.
Akizungumzia kuhusu hali
yake, Nassari alisema amepimwa kipimo cha X-ray ambapo imeonyesha kuwa
pingili za mgongo wake zipo sawa, lakini daktari ameshauri afanyiwe
kipimo kingine kiitwacho MRI ili kuangalia hali ya mishipa kutokana na
maumivu makali anayoendelea kuyapata.
Aidha alitumia fursa hiyo
kumshukuru Mbunge wa Kuteuliwa, Joseph Mbatia kuwa ndiye aliyemsaidia
kufanya mipango kuwasiliana na uongozi wa Bunge na kumwezesha
kuhamishiwa Moi, baada ya wabunge wote wa Chadema kwenda Arusha
kushughulikia waliofariki kwa bomu.
Hata hivyo, Lowassa
alipotafutwa kuhusiana na tuhuma hizo alikataa kuzungumzia suala hilo na
kusema hilo aulizwe Msimamizi wa Uchaguzi, Paulo Kitaleki.
Mwananchi
ilimtafuta Kitaleki ambaye pia ni katibu tarafa, alikanusha kuhusika
kwa Lowassa akielezea kuwa siku ya tukio hilo alikuwa Geita.
“Huyu
Nassari ni mwigizaji na anafaa kuwa msanii kwa kuwa anaigiza tu hata
hakupigwa, bali yeye ndiyo aliyempiga Wakala wa CCM, Hussein Osama
ambaye ni mlemavu, kisha akatimua mbio baada ya vijana kutaka kumkamata,
nashangaa kumwona yupo hospitali akidai kupigwa, siyo kweli,” alisema
Kitaleki.